Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN  yaonya kwa Baraza la Usalama kuhusu athari mbaya za vita kwa wanawake na watoto Ukraine 

Kikao cha Baraza la Usalama likijadili amani na usalama nchini Ukraine.
UN Photo/Manuel Elías
Kikao cha Baraza la Usalama likijadili amani na usalama nchini Ukraine.

UN  yaonya kwa Baraza la Usalama kuhusu athari mbaya za vita kwa wanawake na watoto Ukraine 

Amani na Usalama

Wakati vita nchini Ukraine vimedumu kwa zaidi ya wiki sita, maafisa wawili wakuu wa Umoja wa Mataifa leo wameonya kwenye Baraza la Usalama juu ya maafa makubwa ya vita hivyo kwa wanawake na watoto. 

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Sima Bahous, ambaye amerejea jana Jumapili jioni kutoka Moldova ambako makumi ya maelfu ya Waukraine wamekimbilia, amewaambia wajumbe wa Baraza kwamba ameshuhudia "mabasi yaliyojaa wanawake na watoto ambao wamechoka na wakiwa na hofu kubwa kuwasili kwenye kivuko cha mpakani cha Palanca.” 

UN Women inafanya kazi na washirika wengine wa kibinadamu kuhakikisha kwamba "asili ya kijinsia ya mgogoro huu inashughulikiwa kwa hatua za kijinsia", na kusisitiza kuwa “Hii ni pamoja na kutoa huduma zinazozingatia ulinzi na kukabiliana na ongezeko la kiwewe na mahitaji ya msaada wa kisaikolojia." 

Bi Bahous ameonya kuwa "wanawake wadogo wanalazimika kuzikimbia nyumba zao usiku, familia zilizotenganishwa, hofu ya mara kwa mara ya siku zijazo. Kiwewe hiki kinaweza kuharibu kizazi hiki.” 

Msichana aliyejeruhiwa akiwa kwenye wadi Kyiv, Ukraine baada ya kushambuliwa kwa gari lake.
© WHO/Anastasia Vlasova
Msichana aliyejeruhiwa akiwa kwenye wadi Kyiv, Ukraine baada ya kushambuliwa kwa gari lake.

Madai ya ubakaji 

Mkuu huyo wa UN Women pia amelifahamisha Baraza la Usalama kuhusu madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono. "Madai haya lazima yachunguzwe kwa uhuru ili kuhakikisha haki na uwajibikaji," amesema. 

Pia ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa hatari ya usafirishaji haramu wa binadamu kwani hali inazidi kuwa mbaya, huku wanawake, wasichana na watoto ambao hawajaandamana na wazazi au walezi wakiwa hatarini. 

Bi. Bahous amesisitiza kwamba “Pamoja na kupitia maovu haya yote, wanawake wa Ukraine wanaendelea kutumikia na kuongoza jamii zao na kusaidia wakimbizi wa ndani. Wanawake ni asilimia 80 ya wafanyakazi wote wa afya na huduma za kijamii nchini Ukraine, na wengi wamechagua kutokimbia “amesema. 

 “Mashirika ya wanawake nchini Ukraine hayajaacha kufanya kazi, yakibadili mwelekeo wa kazi zao ili kukidhi mahitaji ya haraka ya watu wanaowahudumia. Na wanafanya hivyo kwa kuhatarisha maisha yao wenyewe,” amesema mkuu wa UN Women, ambaye amesifu ujasiri na uvumilivu wao. 

Pia alikumbusha kuwa wanawake wanaomba "kuwa sehemu ya suluhisho kumaliza mzozo huu. Tunajua kutokana na uzoefu kwamba ushiriki wa wanawake hufanya hatua na ahueni kuwa na ufanisi zaidi na endelevu," 

Aameongeza kuwa  ni muhimu kwamba mashirika ya wanawake yashauriwe na kushirikishwa katika maamuzi yote yanayohusiana na kukabiliana na mgogoro huu unaoendelea. 

Msichana aiyekimbia Ukraine akiwa kwenye kituo cha wakimbizi Poland.
WHO
Msichana aiyekimbia Ukraine akiwa kwenye kituo cha wakimbizi Poland.

Watoto hatarini kukosa chakula cha kutosha 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mipango ya dharura katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, Manuel Fontaine, ambaye alikuwa Ukraine wiki iliyopita, ameeleza kwamba alikuwa ameona mara chache katika kazi yake ya kibinadamu ya miaka 31 "uharibifu mkubwa wa kiasi hicho uliosababishwa kwa muda mfupi sana". 

"Kati ya watoto wanaokadiriwa kuwa milioni 3.2 ambao wamebaki nyumbani hawakukimbia , karibu nusu wako katika hatari ya kukosa chakula cha kutosha. Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mfumo wa usambazaji maji na kukatika kwa umeme kumesababisha takriban watu milioni 1.4 kukosa maji nchini Ukraine. Watu wengine milioni 4.6 wanapata maji kidogo sana," ameliambia Baraza la Usalama. 

Fontaine ameongeza kuwa "Hali ni mbaya zaidi katika miji kama Mariupol na Kherson, ambako watoto na familia zao sasa wamekaa wiki bila maji ya bomba na huduma za vyoo, bila chakula cha kawaida na bila huduma ya matibabu.” 

Bwana. Fontaine amebainisha kuwa mifumo yote inayosaidia watoto kuishi pia inashambuliwa. 

"Mashambulizi dhidi ya hospitali, vituo vya afya na vifaa vya matibabu na mauaji na majeraha ya wataalam wa afya hufanya iwe vigumu zaidi kwa watu kupata huduma za dharura, huduma za afya za msingi na madawa. Mamia ya shule na taasisi za elimu pia zimeshambuliwa au kutumika kwa madhumuni ya kijeshi. Nyingine hutumika kama makazi ya raia. Kufungwa kwa shule nchini kote kunaathiri elimu ya siku zijazo kwa watoto milioni 5.7 wenye umri wa kwenda shule na wanafunzi milioni 1.5 walio katika elimu ya juu" . 

Huku karibu theluthi mbili ya watoto wote wa Ukraine wamekimbia makazi yao katika wiki sita tu za vita, UNICEF na washirika wake wanafanya kila wawezavyo kuwasaidia. 

"Ndani ya Ukraine, tunaendelea kukabiliwa na hali ngumu sana kuendesha shughuli zetu. Tumeona maendeleo katika wiki za hivi karibuni, kwa timu na vifaa vyetu kufikia Sumy, Kharkiv na Kramatorsk, miongoni mwa maeneo mengine. Lakini haitoshi,” amesema afisa huyo wa UNICEF. 

"Uhasama unaoendelea unatuzuia kuwafikia wale wanaohitaji sana katika maeneo mengi ya nchi," aliongeza. 

UNICEF pia husaidia mamlaka za mitaa kutambua na kusajili watoto wasio na wasindikizaji na waliotenganishwa, na kuzipa familia usaidizi wa pesa za kibinadamu. 

Bw Fontaine alisema ana wasiwasi hasa kuhusu kuenea kwa mabaki ya vita ambayo yanawaweka watoto katika hatari ya kifo na majeraha mabaya. Pia alisema UNICEF inafuatilia kwa makini "afya, haki na utu wa wanawake na wasichana, huku hatari ya kunyonywa na kunyanyaswa ikiongezeka". 

Bwana Fontaine amesema ana wasiwasi hasa kuhusu kuenea kwa mabaki ya silaha za vita ambazo zinawaweka watoto katika hatari ya kifo na majeraha ya kutisha. Kwa mantiki hiyo amesema UNICEF inafuatilia kwa makini "afya, haki na utu wa wanawake na wasichana, huku hatari ya ukatili na kunyanyaswa ikiongezeka".