Skip to main content

Miaka mitano ya mzozo Ukraine, zaidi ya shule 750 zimesambaratishwa- UNICEF

Afisa polisi mwenye silaha akiwa doria nje ya jengo la darasa la kwanza ambalo limezingirwa na vifuko vya viroba vya mchanga kuepusha risasi kuingia darasani. Shule hii ipo Marinka eneo la Donetsk Oblast nchini Ukraine
© UNICEF/UN0150811/Gilbertson V
Afisa polisi mwenye silaha akiwa doria nje ya jengo la darasa la kwanza ambalo limezingirwa na vifuko vya viroba vya mchanga kuepusha risasi kuingia darasani. Shule hii ipo Marinka eneo la Donetsk Oblast nchini Ukraine

Miaka mitano ya mzozo Ukraine, zaidi ya shule 750 zimesambaratishwa- UNICEF

Amani na Usalama

Nchini Ukraine, mashambulizi dhidi ya maeneo ya shule yameongezeka mara nne katika robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, imesema taarifa iliyotolewa leo huko Kiev, Ukraine na New York, Marekani ikiongeza kuwa matukio hayo yamesababisha kiwewe kwa wanafunzi na kuwatia hatarini kupata majeraha au kuuawa.

 Ikitolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF taarifa hiyo imesema kati ya mwezi Januari na Aprili mwaka huu, kumekuwepo na mashambulio 12 dhid iya shule ikilinganishwa na mashambulio matatu mwaka jana katika kipindi hicho na kutia hofu juu ya ongezeko hilo na kukumbukshia visa vya mwaka 2017 ambako kulikuwepo na zaidi ya mashambulizi 40.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema “watoto wa shule wanabeba makovu ya kudumu ya kimwili na kiakili kutokana na mzozo unaoendelea nchini Ukraine. Maisha ya kila siku shuleni yanavurugwa na mashambulizi ya makombora na milio ya risasi, ikilazimu watoto kujificha kwenye mahandaki na katika matukio mengi watoto wameingiwa na uoga wa kujifunza.”

Ametolea mfano jinsi ambavyo madarasa yaliyobomolewa kwa makombora yalivyozingirwa na viroba vya mchanga ili kuepusha risasi ziendazo kombo kufikia watoto walio darasani kwa hiyo Bi. Fore amesihi pande zote kinzani kwenye mzozo zihakikishe watoto wako salama.

Tangu mzozo uanze nchini Ukraine mwaka 2014, zaidi ya shule 750 zilizoko pande zote za mapigano zimeharibiwa.

Halikadhalika UNICEF inasihi serikali zote ikiwemo ya Ukraine iridhie azimio la shule salama, ambalo ni azimio la kisiasa kati ya serikali la kuchukua hatua thabiti kulinda wanafunzi, walimu na maeneo ya shule dhidi ya mashambulizi yote ya makusudi kwenye mapigano hayo.

Wiki ijayo, serikali ya Hispani itakuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu shule salama, fursa kwa serikali kuangazia maendeleo yaliyofikiwa katika kutekeleza azimio hilo.