Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita nchini Ukraine inakisukuma ukingoni kizazi cha watoto inaonya UNICEF

Msichana mwenye umri wa miaka 8 akiwa mbele ya jengo huko Irpin, Ukraine ambapo mama yake na dada yake wanaishi pamoja katika chumba kidogo.
© UNICEF/Olena Hrom
Msichana mwenye umri wa miaka 8 akiwa mbele ya jengo huko Irpin, Ukraine ambapo mama yake na dada yake wanaishi pamoja katika chumba kidogo.

Vita nchini Ukraine inakisukuma ukingoni kizazi cha watoto inaonya UNICEF

Amani na Usalama

Takriban mwaka mmoja tangu kushika kasi kwa vita nchini Ukraine hapo 24 Februari 2022, kizazi cha watoto kimepitia miezi 12 ya machafuko, hofu, hasara na misiba. Limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF na kuongeza kuwa hakuna kipengele hata kimoja cha maisha ya watoto hao ambacho mzozo haujakiathiri, kwani watoto wameuawa, kujeruhiwa, kulazimishwa kukimbia nyumba zao, kukosa elimu muhimu na kunyimwa faida za mazingira huru na salama. 

Kupitia taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema "Watoto nchini Ukraine wamepitia mwaka wa kutisha. Mamilioni ya watoto watalala kwenye baridi kali na hofu na wakiamka kwa matarajio ya kuona mwisho wa vita hii kikatili. Watoto wameuawa na kujeruhiwa, na wengi wamepoteza wazazi na ndugu, nyumba zao, shule na viwanja vya michezo. Hakuna mtoto anayepaswa kubeba mateso ya aina hiyo.” 

Ameendelea kusema kwamba mgogoro wa kiuchumi, pamoja na idadi kubwa ya familia zinazoripoti upotevu wa kiwango cha juu cha mapato, pamoja na cyangamoto ya nishati iliyosababishwa na vita vimechangia hali mbaya kwa ustawi wa watoto na familia.  

Changamoto za kiuchumi zimemgusa kila mtu 

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa UNICEF asilimia 80 ya watu waliohojiwa wamebainisha kuzorota kwa hali yao ya kiuchumi, wakati uchambuzi wa shirika hilo ukionyesha kuwa asilimia ya watoto wanaoishi katika umaskini imekaribia mara mbili kutoka asilimia 43 hadi asilimia 82 na hali ni mbaya zaidi kwa watu milioni 5.9 ambao kwa sasa ni wakimbizi wa ndani nchini Ukraine. 

Vita hivyo pia vina athari mbaya kwa afya ya akili na ustawi wa watoto.  

“Takriban watoto milioni 1.5 wako katika hatari ya mfadhaiko, wasiwasi, na msongo wa mawazo wa baada ya kiwewe na masuala mengine ya afya ya akili, yenye uwezekano wa madhara na athari za muda mrefu” Limeongeza shirika hilo. 

Limeendelea kusema kwamba upatikanaji wa huduma za msingi kwa watoto na familia zao umesambaratishwa. 

“Zaidi ya vituo vya afya 1,000 vinaripotiwa kuharibiwa au kusambaratishwa na makombora na mashambulizi ya anga, na mashambulizi kama hayo yakiua na kusababisha majeraha makubwa kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na watoto  na wahudumu wa afya, na kuzuia upatikanaji wa huduma. Maelfu ya watoto wanaokimbia migogoro kote nchini wanakosa chanjo muhimu za kuwakinga na polio, surua, donda koo na magonjwa mengine yanayotishia maisha.” Amesisitiza Bi. Russel 

Katika nyumba yao ya makazi ya Olenivka katika eneo lisilodhibitiwa na serikali la mkoa wa Donetsk, Alika mwenye umri wa miaka 11 na dada yake mwenye umri wa miaka sita Sofia wanaongeza makaa ya mawe kwenye jiko.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Katika nyumba yao ya makazi ya Olenivka katika eneo lisilodhibitiwa na serikali la mkoa wa Donetsk, Alika mwenye umri wa miaka 11 na dada yake mwenye umri wa miaka sita Sofia wanaongeza makaa ya mawe kwenye jiko.

UNICEF na wadau wanashika mkono watoto hao 

Tangu Februari 24 mwaka 2022, UNICEF, kutokana na usaidizi wa jumuiya ya kimataifa, imetoa vifaa vya kujifunzia kwa watoto 770,000, kuwashirikisha watoto milioni 1.4 katika elimu rasmi na isiyo rasmi, kutoa msaada wa afya ya akili na kisaikolojia kwa watoto milioni 2.9 na walezim wao pia inatoa huduma za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto 352,000, inatoa huduma ya maji salama kwa watu milioni 4.6, inatoa huduma za afya kwa watu milioni 4.9, na kutoa msaada wa pesa taslimu kwa madhumuni mbalimbali kwa watu milioni 1.4 ndani ya Ukraine na kaya 47,494 katika nchi jirani. 

 Bi. Russell amesema "Watoto wanahitaji kukomeshwa kwa vita hivi na amani endelevu ili kurejesha utoto wao, kurudi katika hali ya kawaida na kuanza kupona na kujikwamua. Hadi hilo litakapotendeka, ni muhimu kabisa kwamba mahitaji ya afya ya akili na kisaikolojia ya watoto yapewe kipaumbele. Hii inapaswa kujumuisha hatua zinazolingana na umri wao ili kutoa matunzo ya malezi, kujenga mnepo, na haswa kwa watoto wakubwa na vijana, kuwapa fursa ya kutoa maoni yao.” 

Pia amesema vita imevuruga elimu kwa zaidi ya watoto milioni tano, kuwanyima watoto hisia za muundo, usalama, hali ya kawaida na matumaini yanayotolewa na kuwa darasani. Fursa ndogo ya shule inakuja baada ya miaka miwili ya kupoteza bila masomo kutokana na janga la COVID-19, na zaidi ya miaka 8 ya changamoto za elimu kwa watoto wanaoishi mashariki mwa Ukraine. 

Fursa ya kufikisha misaada ni muhimu 

UNICEF inaendelea kutoa wito wa upatikanaji wa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa kuzingatia kanuni, salama, za haraka na zisiozuiliwa, kukomesha mashambulizi dhidi ya watoto na miundombinu wanayoitegemea, ikiwa ni pamoja na shule, hospitali na mifumo ya maji na usafi wa mazingira, kuepuka matumizi ya shule katika mgogoro huu na kukomesha matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi, inayohusika moja kwa moja na mauaji na kulemaza mamia ya watoto.  

Zaidi ya yote, UNICEF inaendelea kuchagiza kukomeshwa kwa uhasama. 

Mwezi Desemba 2022, UNICEF ilizindua ombi lake kla kila mwaka la kibinadamu kwa watoto.  

Shirika hilo linahitaji dola za Marekani bilioni 1.1 kushughulikia mahitaji ya haraka na ya muda mrefu ya watu milioni 9.4, wakiwemo watoto milioni 4, ndani na nje ya Ukraine ambao wameathiriwa sana na vita nchini Ukraine.  

Ufadhili huo utaliwezesha shirika la UNICEF kutoa, kuendeleza na kupanua wigo wa huduma muhimu katika suala la afya, lishe, ulinzi wa watoto, unyanyasaji wa kijinsia, maji na usafi wa mazingira, ulinzi wa kijamii pamoja na juhudi za serikali za misaada na kujikwamua.  

Pia litahakikisha linajiandaa vyema na kwa wakati kwa ajili ya wakimbizi wa ndani wa ziada na harakati za wakimbizi.