Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha hatua ya usitishaji mapigano nchini Afghanistan

Vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa (PPE) vikisambazwa kwa wahudumu wa afya nchini Afgghanistan wakati wa mlipuko wa COVID-19
WHO
Vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa (PPE) vikisambazwa kwa wahudumu wa afya nchini Afgghanistan wakati wa mlipuko wa COVID-19

UN yakaribisha hatua ya usitishaji mapigano nchini Afghanistan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo ameikaribisha hatua ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban kusitisha mapigano ili watu wa Afghanstan waweze kusherehekea sikukuu ya Eid.

Kundi la Taliban limetangaza hii leo kusitisha vita kwa siku tatu wakati wa sikukuu za Eid al-Fitr na rais wa Afghanistan akatoa mari kwa vikosi vya usalama pia kusitisha mapigano kwa siku hizo tatu isipokuwa pale tu watakaposhambuliwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezisihi pande zote kuitumia fursa hii na kuunga mkono mchakato wa amani unaoongozwa na Afghanistan.

Bwana Guterres amesisitiza, “ni suluhisho la amani pekee ambalo linaweza kumaliza mateso ya watu wa Afghanistan. Umoja wa Mataifa umejizatiti kusaidia juhudi hizo muhimu za serikali ya Afghanistan na watu wake.”

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA nao kupitia mitandao ya kijamii umekaribisha hatua hii ya kusitisha mapigano kwa ajili ya sikukuu ya Eid al-Fitr kwa kusema kuwa, watu wa Afghanistan, “wanapaswa kupumua kutoka kwenye vurugu hizi” na wakazisihi pande zote, “kuzingatia usitishaji mapigano na kutafuta njia za kufanya tukio hili la usitishaji mapigano kuwa la kudumu.Mazungumzo ya amani kati ya watu yanapaswa kuanza.”

Tweet URL

 

Taliban walitiliana saini ya makubaliano ya amani na Umoja wa Mataifa tarehe 29 mwezi Februari ya mwaka huu wa 2020. Kisha serikali ya Afghanistan iliamuru vikosi vya usalama kubadili hali na badala yake kuwa ya kujilinda na kuweka mazingira ya mazungumzo ya amani. Hata hivyo, matukio ya vurugu yamekuwa yakitokea mara kwa mara na idadi ya mashambulizi kwa vikosi vya usalama na raia yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.

Mnamo tarehe 12 ya mwezi huu wa Mei, shambulizi la kigaidi kwenye hospitali ya akina mama kujifungua pamoja na eneo la maziko nchini Afghanistan yaliua takribani watu 42. Ingawa kundi la Taliban lilikataa kuhusika na tukio hili, Rais wa Afghanistan bado aliamuru vikosi kuanza operesheni Kali ya kupambana na Taliban na makundi mengine.