Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunatembea tukiwa usingizini wakati wa kukabili  uchafuzi wa hali ya hewa: Guterres

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unasababisha mabadiliko ya tabianchi.
© Unsplash/Ella Ivanescu
Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unasababisha mabadiliko ya tabianchi.

Tunatembea tukiwa usingizini wakati wa kukabili  uchafuzi wa hali ya hewa: Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati mabishano baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea yakiendelea juu ya uchafuzi wa tabaka la ozoni na nani amefanya nini katika kupunguza uchafuzi huo, hali ya hewa inazidi kuwa mbaya na joto likizidi kuongezeka duniani kote.

Akizungumza katika mkutano wa uchumi endelevu uliowakutanisha wakuu wa nchi na serikali hii leo, Guterres amesema amekaribishwa kuzungumzia mada ya “kuhakikisha tunasalia na nyuzi joto 1.5 na hatima ya Sayari yetu” lakini ukweli ni kuwa tafiti mbalimbali zinazotolewa na ushahidi unaonesha lengo hili lipo mbioni kushindikana kutekelezeka kwa kuwa lengo hilo lipo mahututi katika chumba cha wagojwa.

Amesema mkutano wa mazingira uliofanyika mwaka jana jijini Glasgow Scotland ulikuja na ahadi za kuvutia ikiwemo “Kupunguza ukataji miti, uchafuzi wa hewa, kuhimiza mashirika ya Kifedha ya Kimataifa kuzingatia udhaifu wa hali ya hewa katika usaidizi wao, pamoja na mengine mengi lakini changamoto kubwa haikutatuliwa, haikushughulikiwa vizuri kwakuwa changamoto hiyo ni pengo kubwa la uzalishaji wa hewa ukaa”

Tunatembea tukiwa usingizini

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema sayansi haiongopi na inaonesha namna joto linavyozidi kuongezeka na tatizo linazidi kuwa baya.

“Kulingana na ahadi za sasa za kitaifa, uzalishaji wa hewa chafuzi duniani unatarajiwa kuongezeka kwa karibu asilimia 14 katika kipindi hiki cha miaka ya 2020 na kuendelea lakini mwaka jana pekee, uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na nishati duniani ulikua kwa asilimia 6 hivi ni viwango vyao vya juu zaidi katika historia” amesema Guterres na kuongeza kuwa “ uzalishaji wa makaa ya mawe nao umeongezeka hadi kuweka rekodi ya viwango vya juu zaidi, tunatembea tukiwa tumelala kwa hili la uharifubu wa hali ya hewa.”

Nini kifanyike

Akizungumzia namna bora ya kushughulika na tatizo hili amesema ni vyema nchi zilizoendelea na zinazoendelea kuacha kuendelea kutupiana lawama ya nani amefanya nini katika kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na badala yake kuendelea na juhudi za kupunguza uharibifu huu ambao wiki mbili zilizopita ripoti mpya ya jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi “IPCC ilithibitisha kuwa nusu ya wanadamu tayari wanaishi katika eneo la hatari huku mataifa ya visiwa vidogo, nchi zilizoendelea na watu maskini na walio hatarini kila mahali wakiwa kwenye mstuko wa hali ya hewa.”

Amesisitiza kuwa Katika ulimwengu uliounganishwa kimataifa, hakuna nchi na hakuna shirika, lm kujikinga na viwango hivi vya machafuko na ndio maana ni busara kushirikiana katika kuleta suluhu ya kudumu.

“Nimekuwa nikihamasisha kuundwa kwa miungano ili kutoa rasilimali na teknolojia kwa mataifa makubwa yanayoibukia kiuchumi ili kuharakisha mabadiliko yao ya matumizi kutoka kwa makaa ya mawe hadi nishati mbadala.”

Amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa na kutolea mfano “ Nchi zilizoendelea, benki za maendeleo za kimataifa, taasisi za kifedha za kibinafsi na makampuni yenye ujuzi wa kiufundi  kwa pamoja zinahitaji kuunganisha nguvu katika miungano hii ili kutoa msaada kwa kiwango kikubwa na kwa kasi kwa uchumi unaotumia makaa ya mawe. Muungano wa aina hiyo umeundwa nchini Afrika Kusini.”

Amewaeleza wakuu wa nchi katika mkutano huo kuwa changamoto wanayopaswa kuishughuliak kwa sasa kuwa wanahitaji kuwa na hali ya udharura zaidi kuhusu mifumo hiyo ya ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kiuchumi ili kuhakikisha kuwa nchi zote za G20 zinapunguza uzalishaji wa hewa ukaa.