Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakbali bora unawezekana endapo tutachukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi sasa: IPCC Ripoti

Umeme unaozalishwa na mashamba ya upepo hupunguza utegemezi wa nishati inayotumia makaa ya mawe.
© Unsplash/Fabian Wiktor
Umeme unaozalishwa na mashamba ya upepo hupunguza utegemezi wa nishati inayotumia makaa ya mawe.

Mustakbali bora unawezekana endapo tutachukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi sasa: IPCC Ripoti

Tabianchi na mazingira

Ripoti iliyotolewa na Jopo la Umoja wa Mataifa  linalohusika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi (IPCC), inaelezea chaguzi nyingi ambazo zinaweza kuchukuliwa sasa, ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu.

Tathimini ya ripoti hiyo, "Mabadiliko ya tabianchi 2023: Ripoti ya Muundo", iliyotolewa leo kufuatia kikao cha wiki moja cha IPCC huko Interlaken, inatanabaisha kwa umakini mkubwa juu ya hasara na uharibifu unaopatikana sasa, na unaotarajiwa kuendelea hadi siku zijazo, ambao unaathiri vibaya watu walio hatarini zaidi na mifumo ikolojia.

Kwa mujibu wa ripoti Joto tayari limepanda hadi nyuzi joto 1.1 zaidi ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, matokeo ya zaidi ya karne moja ya kutumia nishati ya mafuta kisukuku, pamoja na matumizi ya nishati na ardhi yasiyo na usawa na yasiyo endelevu.

“Hii imesababisha matukio ya mabadiliko ya tabianchi ya mara kwa mara na mabaya zaidi ambayo yamesababisha athari hatari kwa asili na watu katika kila pembe ya dunia.”

Ukosefu wa uhakika wa chakula na maji unaotokana na mabadiliko ya tabianchi na  unatarajiwa kuongezeka sanjari na ongezeko la joto na ripoti inasema hatari hizi zinapounganishwa na matukio mengine mabaya, kama vile magonjwa ya milipuko au migogoro, huwa vigumu zaidi kuzidhibiti.

Wafanyakazi kutoka PHILERGY, muuzaji kutoka Ujerumani-Ufilipino na kisakinishi cha nishati ya jua, wakifunga paneli za jua katika nyumba huko Manila, Ufilipino.
IMF/Lisa Marie David
Wafanyakazi kutoka PHILERGY, muuzaji kutoka Ujerumani-Ufilipino na kisakinishi cha nishati ya jua, wakifunga paneli za jua katika nyumba huko Manila, Ufilipino.

Muda ni mfupi, lakini kuna mwelekeo wa mustakbali

Ripoti hiyo inasema endapo halijoto itawekwa hadi nyuzi joto 1.5 zaidi ya viwango vya kabla ya mapindunzi ya viwanda, upunguzaji wa hewa chafuzi wa kina, haraka na endelevu utahitajika katika sekta zote muongo huu.

“Uchafuzi unahitaji kupungua sasa, na upunguzwe kwa karibu nusu ifikapo 2030, ikiwa lengo hili lina nafasi yoyote ya kuafikiwa.”

Suluhisho lililopendekezwa na IPCC ni "maendeleo yanayohimili mabadiliko ya tabianchji," ambayo yanahusisha kuunganisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hatua za kupunguza au kuepuka utoaji wa gesi chafuzi kwa njia zenye ufanisi mkubwa.

Mifano ni pamoja na upatikanaji wa nishati safi, umeme wenye hewa ukaa ndogo, usafiri usiozalisha hewa ukaakabisa au hewa ukaa ndogo na uboreshaji wa hewa, faida za kiuchumi kwa afya ya watu kutokana na uboreshaji wa hewa pekee zingekuwa takriban sawa, au labda kubwa zaidi, kuliko gharama za kupunguza au kuzuia uzalishaji huo.

Christopher Trisos, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo  amesema "Mafanikio makubwa zaidi katika ustawi yanaweza kuja kutokana na kuweka kipaumbele katika kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii zenye kipato cha chini na zilizotengwa, ikiwa ni pamoja na watu wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi. Hatua za kasi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zitakuja tu ikiwa kuna ongezeko kubwa la ufadhili wa fedha. Ukosefu wa fedha na kutokuwa na mipango mizuri kunarudisha nyuma maendeleo."

Serikali ni muhimu

Ripoti hiyo imesisitiza kuhusu uwezo wa serikali wa kudhibiti vizuizi vya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kupitia ufadhili wa umma na ishara za wazi kwa wawekezaji, na kuongeza hatua za sera zilizojaribiwa.

Mabadiliko katika sekta ya chakula, umeme, usafiri, viwanda, majengo na matumizi ya ardhi yameelezwa kama njia muhimu za kupunguza utoaji wa hewa chafu, pamoja na kuhamia katika matumizi yalsiyozalisha hewa ukaa, ambayo yangeboresha afya na ustawi.

Mwenyekiti wa IPCC Hoesung Lee  kwa upande wake amesema "Mabadiliko ya kimfumo yana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa pale ambapo kuna uaminifu, ambapo kila mtu anafanya kazi pamoja kuweka kipaumbele katika kupunguza hatari, na pale ambapo manufaa na mizigo inabebwa kwa usawa.”

Ameongeza kuwa "Ripoti hii ya muhtasari inasisitiza uharaka wa kuchukua hatua kabambe zaidi na inaonyesha kwamba, ikiwa tutachukua hatua sasa, bado tunaweza kupata mustakabali bora na endelevu kwa wote."

Mradi wa Umeme wa Mvuke wa Muara Laboh unasaidia kuendeleza Indonesia kuelekea malengo yake ya nishati mbadala na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
ADB/Gerhard Joren
Mradi wa Umeme wa Mvuke wa Muara Laboh unasaidia kuendeleza Indonesia kuelekea malengo yake ya nishati mbadala na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Guterres atangaza mpango wa kutozalisha hewa ukaa

Katika ujumbe wa video uliotolewa leo kuhusu ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameilezea ripoti hiyo kama "jinsi ya mwongozo wa kutegua bomu la wakati wa mabadiliko ya tabianchi."

Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinahitajika katika nyanja zote amesema  "kila kitu, kila mahali, kwa wakati mmoja," akimaanisha kama mshindi wa tuzo ya Academy ya filamu bora mwaka huu.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amependekeza kwa kundi la G20 ambalo ni la nchi zilizoendelea kiuchumi duniani  "Mkataba wa mshikamano wa mabadiliko ya tabianchi," ambapo watoaji hewa chafuzi wote wakubwa watafanya juhudi za ziada kupunguza uzalishaji, na nchi tajiri zitakusanya rasilimali za kifedha na kiufundi kusaidia nchi zinazoibukia katika juhudi za pamoja ili kuhakikisha kuwa viwango vya joto duniani havipandi kwa zaidi ya nyuzi joto 1.5 zaidi ya viwango vya kabla ya kuanza kwa maendeleo ya viwanda.

Bwana Guterres ametangaza kuwa anawasilisha mpango wa kuongeza juhudi za kufanikisha mkataba huo kupitia “Agenda ya kuharakisha mchakato”, ambayo inahusisha viongozi wa nchi zilizoendelea wanaojitolea kufikia hatua ya kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2040, na nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2050.

Ajenda hiyo inataka kukomesha uzalishaji wa makaa ya mawe, uzalishaji wa umeme usio na hewa ukaa ifikapo mwaka 2035 kwa nchi zote zilizoendelea na 2040 kwa dunia nzima, na kusitishwa kwa utoaji wa leseni au ufadhili wa mafuta kisukuku na gesi mpya, na upanuzi wowote wa mafuta na mafuta yaliyopo, pia hifadhi ya gesi.

Hatua hizi, ameendelea kusema Bwana Guterres, “lazima ziambatane na ulinzi kwa jamii zilizo hatarini zaidi, kuongeza fedha na uwezo kwa ajili ya kukabiliana na hasara na uharibifu, na kuendeleza mageuzi ili kuhakikisha benki za maendeleo ya kimataifa zinatoa misaada na mikopo zaidi, na kuhamasisha kikamilifu fedha binafsi.”

Akiangalia mbele kwa mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaotarajiwa kufanyika Dubai kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Disemba, Bwana Guterres amesema kuwa anatarajia viongozi wote wa G20 wawe wamejitolea kuchangia mchango mkubwa wa kitaifa uliodhamiriwa na uchumi mpya unaojumuisha gesi zote zinazochafua mazingira, na kuonyesha malengo yao kukata kabisa uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2035 na 2040.