Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko vijana wa New Zealand, dunia tuzingatie mambo manne katika mabadiliko ya tabianchi- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika jopo la vijana na uongozi wa jamii ya watu wa visiwa vya Pasifiki.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika jopo la vijana na uongozi wa jamii ya watu wa visiwa vya Pasifiki.

Heko vijana wa New Zealand, dunia tuzingatie mambo manne katika mabadiliko ya tabianchi- Guterres

Tabianchi na mazingira

Vijana nchini New Zealand wamepongezwa na Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri na mchango wao mkubwa katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi , huku wakiaswa kuongeza juhudi na kuwa wabunifu Zaidi kwa kusaka suluhu mbadala kwa ajili ya changamoto hii inayoighubika duniani.

Pongezi hizo kwa vijana wa New Zealand zimetolewa leo na, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alipozungumza na jopo la vijana na uongozi wa jamii ya watu wa visiwa vya Pasifiki kwa jitihada zao za kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika siku ya pili ya ziara yake katika hotuba yake amepongeza uongozi wa vijana  

Bw. Guterres amesema juhudi za  Generation Zero, shirika lisilo la kiserikali linaloongozwa na  vijana wa New Zealand katika kutoa suluhisho kwa nchi ili kupunguza uchafuzi  wa hewa ukakaa kupitia usafiri mbadala, miji salama, kuishi bila kutegemea  mafuta ni juhudi chanya ambazo zinazongesha mbele ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa inahitaji kutiliwa mkazo na kupewa kipaumbele na kila mtu.

Halikadhalika mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa  amesema vijana wanaweza kusaidia kuhakikisha kwamba "tunaweza kufikia lengo letu kuu, la kutokuwa na ongezeko la joto Zaidi ya nyuzi joto 1.5 mwishoni mwa karne hii. Nina uhakika kuwa vijana duniani kote wataweza kuwafikishia serikali zao ujumbe huu”

Ili kufikia muafaka huo Bw guterres amependekeza hatua nne, katika mapambano ya haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambazo ni ;“Mosi kuhamisha kodi kutoka kwenye mishahara na kuihamishia kwenye bidhaa zinazozalisha hewa ukakaa, akisema toza kodi uchafuzi wa mazingira sio watu , Pili kukomesha ruzuku kwa sekta ya mafuta kwani fedha za walipa kodi hazipaswi kuchagiza vimbunga, kusambaza ukame na ongezeko la joto, kuyeyusha theluji na kubabua matumbawe, tatu kuacha  ujenzi mpya wa viwanda vya  makaa ya mawe ifikapo mwaka wa 2020 na nne tunahitaji uchumi unaojali mazingira na sio unaoyasambaratisha.”

Amesisitiza kuwa ni muhimu sana kuzishawishi serikali kwamba lazima zichukuwehatua sasa kwani   kuna changamoto kubwa katika kutekeleza haya, akitolea mfano upinzani aliokutana nao mwaka  2018 wa kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi, COP24.  Akisema,  kuna baadhi ya serikali ambazo zinasuwasuwa kuchuwa hatua katika suala la mabadiliko ya hali yatabianchi huku  wakisahau kuwa gharama za athari ni kubwa zaidi kuliko gharama yoyote watakayoitumia sasa kwa  hatua za watakazochukua hivi sasa kudhibiti mtihani huu.