Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi rangi watia sumu kwenye taasisi na jamii - Guterres

Raia wa Panama wenye asili ya Afrika wanatumia sauti zao kutokomeza ubaguzi wa rangi na ubaguzi.
UN Panama/Javier Conte
Raia wa Panama wenye asili ya Afrika wanatumia sauti zao kutokomeza ubaguzi wa rangi na ubaguzi.

Ubaguzi rangi watia sumu kwenye taasisi na jamii - Guterres

Haki za binadamu

Ubaguzi umeendelea kutia sumu kwenye taasisi, miundo ya kijamii na katika maisha ya kila siku, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo wakati wa mkutano maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York, Marekani juu ya kile kinachoitwa kuwa kichocheo cha kuhalalisha chuki, kupinga utu na kusambaza ghasia.
 

Mkutano huo umefanyika mahsusi kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi siku ambayo hata hivyo itaadhimishwa duniani kote tarehe 21 mwezi huu wa Machi.

“Ubaguzi unaendelea kuwa kichocheo cha ukosefu wa usawa unaoendelea kuota mizizi, unanyima watu haki ya msingi ya binadamu,” amesema Guterres akifafanua kuwa ubaguzi wa rangi unaendelea kuvuruga na kukosesha jamii duniani kote utulivu.

Ubaguzi unakandamizi demokrasia, unamomonyoa uhalali wa serikali na kukwamisha harakati za kuibuka kutoka kwenye janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 kwa ujumuishi na uendelevu.

Guterres amesema siku ya maadhimisho ya kupinga ubaguzi duniani ni siku ya kutambua na kutoa wito wa dharura wa kuchukua hatua.

Uhusiano usiopingika

Katibu Mkuu amegusia uhusiano baina ya ubaguzi wa rangi, ukosefu wa usawa kijinsia akitaja muingiliano na uhusiano wa ubaguzi unaokumba wanawake Weusi na makundi madogo.
Zaidi ya  yote, “hakuna nchi ambayo inaweza kusema haiwezi kuathirika na ukosefu wa stahmala au chuki.”

“Waafrika na watu wenye asili ya Afrika, waasia na wale wenye asili ya bara la Asia, jamii za makundi madogo, watu wa jamii ya asili, wakimbizi, wahamiaji na wengine wengi, wote wanaendelea kukabiliana na unyanyapaa, visingizio, ubaguzi na ghasia.”

Bado naamini kwenye jiji la New York: Mchoro wa msanii unaopinga ubaguzi kwa watu wa Asia
UN Video
Bado naamini kwenye jiji la New York: Mchoro wa msanii unaopinga ubaguzi kwa watu wa Asia

‘Mwamba’ wa jamii

Ujumbe wa mwaka huu, “Sauti dhidi ya ubaguzi wa rangi” unatoa wito kwa kila mtu kusikiliza kwa makini, kupaza sauti kubwa na kuchukua hatua.

“Sote tuna wajibu wa kuwajibika kwa mshikamano na harakati za usawa na haki za binadamu kila mahali. Na  lazima tuoneshe mshikamano wetu na wale wote wanaokimbia mapigano na mizozo,” amesema Katibu Mkuu akisihi dunia kupaza sauti dhidi ya kauli za chuki hadharani na kwenye mitandao.

Amepigia chepuo umuhimu wa kutetea fursa za raia kwa kulinda uhuru wa kujieleza na kukutana akieleza kuwa huo ndio mwamba wa jamii zenye demokrasia, amani na ujumuishi.

 “Unyanyapaa husababisha habari potofu na ubaguzi. Hiyo inatuzuia kusonga mbele. " Clara, 23, Hispania
© UNICEF/@witchtropolis
“Unyanyapaa husababisha habari potofu na ubaguzi. Hiyo inatuzuia kusonga mbele. " Clara, 23, Hispania

‘Vunjeni mifumo ya kibaguzi’

Bwana Guterres ametoa wito wa kuwepo kwa makubaliano ya kijamii kuhusu haki na kushughulikia umaskini, ujumuishi, kuwekeza kwenye elimu, na kujenga upya imani na mtangamano wa kijamii.

“Lazima tusikilize wale ambao wanakabiliwa na ukosefu wa haki, na kuhakikisha shaka na shuku zao pamoja na matakwa yao yanakuwa kitovu cha juhudi za kuvunja mifumo ya kibaguzi,” amesisitiza Katibu Mkuu.

Rais wa UNGA apazia sauti Ukraine

Akiongoza mkutano huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, Abdulla Shahid alianza kwa kuelezea hofu yake kubwa juu ya ghasia dhidi ya raia hususan wanawake na watoto nchini Ukraine.
Kadri familia zinavyoendelea kukikimbia kusaka hifadhi na usalama katika maeneo mapya, “fikra zetu ziko na wananchi wa Ukraine.”
Lengo halijafikiwa
Tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa kupinga kwa ubaguzi wa rangi zaidi ya nusu karne iliyopita, bado harakati za kutokomeza ubaguzi zinayoyoma, Bwana Shahid amekumbusha washiriki.

Licha ya mkataba huo kuwa unakaribia kuwa umeridhiwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, “bado tunaendelea kushuhudia ongezeko la kauli za chuki, ukosefu wa stahmala na ubaguzi wa rangi hasa kwa makundi madogo.”

“Kushindwa kwetu kimaadili kutokomeza ubaguzi wa rangi ni kushindwa dhidi ya kila kitu tunachosimamia katika ukumbi huu,” amesema Bwana Shahid.

Ametamatisha akisema, “hebu na nielekewe: Ubaguzi wa rangi ni fikra potofu iliyo wazi na jambo linaloibuka kutoka kwenye kauli za chuki na propaganda za chuki.”