Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine: Turejee kwenye diplomasia na mazungumo – Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akiwa ndani ya  ukumbi wa Baraza hilo
UN/Eskinder Debebe
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akiwa ndani ya ukumbi wa Baraza hilo

Ukraine: Turejee kwenye diplomasia na mazungumo – Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Amani na Usalama

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akizungumzia hali inayoendelea Ukraine, ametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja na kurejea katika diplomasia na mazungumzo.  

Bwana Shahidi katika ujumbe alioutuma kupitia msemaji wake jioni ya Alhamis hii jijini New York, Marekani, amesema, “Mkataba wa Umoja wa Mataifa unasimama katika msingi wa kanuni ya usawa wa uhuru na unatoa wito kwa Nchi Wanachama kusuluhisha mizozo yao ya kimataifa kwa njia za amani bila vitisho au matumizi ya nguvu dhidi ya ukamilifu wa himaya au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote.” 

Kiongozi huyo ameeleza kuwa mashambulizi ya kijeshi yanayoendelea kufanywa na Urusi nchini Ukraine hayaendani na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kwa msingi huo anaurudia wito wake kwa Nchi Wanachama zote kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu. 

“Ninatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja, kupunguzwa kwa mivutano na kurejea kwa uthabiti kwenye diplomasia na mazungumzo.” Amesema. 

Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amehitimisha taarifa yake fupi akizungumzia suala la ufikiaji wa usaidizi wa kibindamu kwa Ukraine na watu wake kuwa ni suala la kipaumbele na hitaji la wakati huu.  

TAGS: Abdulla Shahid, UNGA76, Abdulla Shahid, Russia, Urusi, Ukraine, Vladimir Putin