Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiswahili ni chachu ya kusongesha ajenda za UN – Guterres

Maadhimisho ya kwanza ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. (Wa pili kushoto)  ni Balozi Kennedy Gastorn, Mwakilishi wa  kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
UN/ Manuel Elias
Maadhimisho ya kwanza ya siku ya Kiswahili duniani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. (Wa pili kushoto) ni Balozi Kennedy Gastorn, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.

Kiswahili ni chachu ya kusongesha ajenda za UN – Guterres

Utamaduni na Elimu

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema lugha ya Kiswahili imekuwa chachu ya kusongesha ajenda nyingi za Umoja wa Mataifa ikiwemo ile ya maendeleo ya maendeleo endelevu, SDGs sambamba na ile ya Muungano wa Afrika, ajenda 2063.

Guterres amesema hayo leo jijini New York, Marekani kupitia msemaji wake Stephane Dujarric katika ujumbe wake wa siku ya leo ambayo ni siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili.

“Hapa Umoja wa Mataifa kama mnavyofahamu, tuna taarifa nzuri sana zinazochapishwa kwenye mtandao kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, mitandao ya kijamii na redio ikihudumia wazungumzaji wa kiswahili na wale wanaotaka kujifunza,” amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa “leo ni siku muhimu sana kwa kuwa Kiswahili kinazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 na miongoni mwa lugha zinazozungumzwa zaidi barani Afrika, na lugha hii ina asili ya Afrika.”

Kutambuliwa kwa Kiswahili ni kumuenzi Mwalimu Nyerere- Rais GA

Wakati huo huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdullah alihutubia washiriki kwa njia ya video akisema, “kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili ni muhimu sana kwa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwa kuzingatia idadi ya wazungumzaji wa lugha hiyo na maeneo ambako inazungumzwa zaidi kusini mwa jangwa la Sahara.”

Amesema lugha ya kiswahili ni chombo muhimu sana kwenye maendeleo, utambulisho na pia mazungumzo baina ya jamii mbalimbali, bila kusahau ujumuishi katika jamii.

Amemtaja Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere akisema, “marafiki zangu tarehe 7 mwezi Julai mwaka 1954, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya harakati za uhuru.”

Bwana Shahidi amesema, “kwa kutambua Kiswahili kama lugha ya mawasiliano duniani, tunamkumbuka yeye na napongeza Umoja wa Mataifa kwa kutambua Kiswahili kama lugha ya ujenzi wa amani na mhimili wa tamaduni mbalimbali.”