Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli za chuki sio uhuru wa kuongea, ni ubaguzi: UN

Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifajijini New York Marekani
UN/Eskinder Debebe
Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifajijini New York Marekani

Kauli za chuki sio uhuru wa kuongea, ni ubaguzi: UN

Masuala ya UM

Chuki dhidi ya Wayahudi bado ipo na ni moto unaoendelea kuwaka bila kuwepo dalili zinazoonekana za kuuzima, ameonya leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres .

Katibu Mkuu ameyasema hayo akizungumza katika mkutamo wa Baraza Kuu kuhusu kukabiliana na chuki dhidi ya Wayahudi na mifumo mingine ya ubaguzi wa rangi na chuki ikiwa ni pamoja na changamoto za kuelimisha kuhusu kuvumiliana na kuheshimiana katika zama hizi za kidijitali.

Amesema kwa mujibu wa utafiti uliotolewa mwezi uliopita katika ripoti ya chuo kikuu cha Tel Aviv idadi ya matukio ya kikatili ya chuki dhidi ya Wayahudi yameongezeka kwa asilimia 13 mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.

“Marekani, Ulaya na kwengineno mashambulizi dhidi ya Masinagogi, mkaburi na watu binafsi yameendelea kuwafanya Wayahudi kuwa na hofu kubwa. Katika enzi hizi chuki za zamani zinaonekana kushika usukani, na zaidi ya hapo kutovumiliana imekuwa ni jinamizi linaloongozwa na watu wengi”

Hali halisi ya chuki

Guterres ameongeza kuwa katika miezi ya karibuni katika sehemu mbalimbali duniani mbali ya mashambulizi kwenye Masinagogi tumeshuhudia mauaji misikitini na mashambulizi ya mabomu makanisani.

Wahamiaji na wakimbizi wanaendelea kukabiliwa na upinzani na ukatili, wafuasi wa itikadi za watu weupe ndio kuonekana wa maana kuliko wengine zinaongezeka na sera za kinazi zinajipenyeza kwenye masuala ya uchaguzi na kuonyesha ujumbe wa kibaguzi.

Katibu Mkuu amesema na katika zama hizo za kidijitali kuna wimbi kubwa na mabalozi wa kusambaza chuki kwenye majukwaa mapya ambayo watu wenye itikadi Kali wanaweza kukutana na kuchagizana.

María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani
UN /Manuel Elias
María Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani

Amesisitiza kuwa “juhudi zetu zinahitaji kuongezeka haraka katika zama hizo za kidijitali ambapo chuki inashamiri. Mitandao ya kijamii inatumika kuogofya jamii na kuathiri watu mara nyingi wanawake , jamii za wachache na wasiojiweza. Mitandao ya kijamii inaweka mazingira ya chuki kutapakaa kwa kiwango kikubwa, bila gharama wala uwajibikaji, na hivyo kuwavutia wenye dhamira mbaya.” 

  Wadau wengine

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa akiunga mmono kupinga hali hii amesema kinyume chau pendo si chuki bali ni kutofautiana akimnukuu mmoja wa washairi maarufu duniani Elie Visel.

Bi Espinosa amesema “Mashambulizi haya  na chuki dhidi ya Wayahudi ni kitendo kisichokubalika lakini chakusikitisha zaidi si ya kushangaza , na tunajua nini kinachoweza kutokea endapo chuki haitodhibitiwa, tumeshuhudia mauaji ya kimbari Rwanda na manazi walikatili maisha ya Wayahudi milioni 6 wakati wa Holocoast, hatua madhubuti zinahitaji kuchukuliwa sasa la sivyo dunia inaelekea kubaya.”

Adama Dieng mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari
UN Photo/Manuel Elías
Adama Dieng mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari

Akisisitiza aliyoyasema Katibu Mkuu Rais wa Baraza Kuu amesema “Tunahitaji kuwekeza katika mshikamano wa kijamii ili watu wote katika jamii wahisi kwamba  asili yao na utaifa wao unaheshimika na kwamba wana sauti katika mustakabali wa jamii zao. Hebu tuwe wazi kwamba hotuba za chuki sio uhuru wa kuongea ni ubaguzi”

Akisistiza kuhusu kukata mzizi wa hotuba za chuki, mwashauri maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya kimbari Adama dieng akukumbusha kwamba hotuba za chuki ndio chanzo cha zahma. " wote lazima tukumbuke kwamba uhalifu wa chuki unatokana na hotuba za chuki, wote lazima tukumbuke kwamba mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi Rwanda yalichochewa na hotuba za chuki. Mauaji ya Holocoast hayakuanza na vyumba vyenye gesi , yalianza mapema kabla ya hapo na hotuba za chuki na tunayoyashuhudia Myanmar dhidi ya Warohingya yalianza na pia na hotuba za chuki. Na leo hii tunayoyashuhudia kote duniani , ya kuongezeka kwa itikadi kali, kila mahali wanavyotendewa wakimbizi na wahamiaji, kuibuka kwa makundi ya unazi na ubaguzi sasa tunachohitaji ni kufanya kila liwezekanalo kushughulikia hotuba za chuki.