Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 11 ya vita ya Syria, Guterres asema “tuchague amani”

Majengo yaliyoharibiwa kwa makombora kwenye mji wa mashariki wa Aleppo nchini Syria. Yadaiwa silaha za kemikali zilitumika kwenye mashambulizi.
OCHA/Halldorsson
Majengo yaliyoharibiwa kwa makombora kwenye mji wa mashariki wa Aleppo nchini Syria. Yadaiwa silaha za kemikali zilitumika kwenye mashambulizi.

Miaka 11 ya vita ya Syria, Guterres asema “tuchague amani”

Amani na Usalama

Mwaka mwingine umepita! Kumbukizi ya kutisha ya vita iliyosambaratisha Syria na watu wake! Ndivyo anavyoanza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa miaka 11 tangu kuanza kwa vita nchini Syria.

 

Katibu Mkuu amesema kipindi hicho kimekuwa cha mapigano ya kikatili ambayo yamekuwa na gharama isiyopimika kwa binadamu kwa kuwa wasyria wamegubikwa na ukiukwaji wa kiwango cha juu kabisa  wa haki za binadamu.

“Uharibifu ambao wasyria wamepitia ni wa kiwango kikubwa na mbaya zaidi unaoweza kulinganishwa na matukio katika historia ya zama za dunia ya sasa,” amesema KAtibu Mkuu.

Guterres amesema katu kusiweko na ukwepaji wa sheria akiongeza “uharibifu ambao vita hiyo imesababisha kwenye miundombinu umeongeza janga la kiuchumi na kufanya mahitaji ya kibinadamu kufikia cha juu zaidi tangu kuanza kwa mzozo huo wa kivita.”

Mamilioni ya wakimbizi wa ndani na wakimbizi wanahaha kuishi katika mazingira magumu. 

Baada ya kimbunga Norma, hali ya baridi kali imeathiri sana wakimbizi wa Syria nchini Lebanon
© UNHCR/Diego Ibarra Sánchez
Baada ya kimbunga Norma, hali ya baridi kali imeathiri sana wakimbizi wa Syria nchini Lebanon

Nini kifanyike?

Guterres anasema “katu hatupaswi kukata tamaa. Tunapaswa kuchukua  hatua sasa. Lazima tuoneshe ujasiri na azma ya kuchukua hatua zaidi ya kauli za hovyo ili kuleta amani na kuchukua hatua zote ili kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa MAtaifa namba 2254 la mwaka 2015 kuhusu suluhu ya kisiasa Syria inayoongozwa na wasyria wenyewe.”

Katibu Mkuu amesema njia hiyo ndio suluhu inayoweza kukidhi matamanio ya wasyria, halikadhalika kuweka mazingira chanya kwa raia wa Syria walio ukimbizi kurejea nyumbani kwa hiari, katika mazingira ya ut una kwa usalama.

Halikadhalika njia hiyo amesema itawezesha kukabiliana na ugaidi, kuheshimu mamlaka ya Syria na uhuru wake.

Pamoja na hatua hizo Katibu Mkuu amesema ni lazima kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafikia wahitaji huku akisema hatua za Syria kujikwamua nazo zipatiwe kipaumbele huku mahitaji ya kuokoa maisha yakizingatiwa kwa kujenga mnepo kwa wananchi.

Tuchague amani

Kwa Baraza la  Usalama, Katibu Mkuu ametoa wito lifikie muafaka katika kuongeza tarehe 1 mwezi Julai mwaka huu muda wa azimio namba 2585 la mwaka 2021 akisema ni wajibu na maadili ya kibinadamu.

Azimio hilo linaridhia matumizi ya mpaka wa Bab al-Hawa katika kuvusha misaada ya kibinadamu ambapo mpaka huo ni wa kimataifa kati ya Syria na Uturuki.

“Juhudi zetu za pamoja zinahitajika ili kumaliza vitendo vya ukamatwaji holela na kutoweshwa kwa watu makumi ya maelfu. Ni wakati wa kujibu wito wa dharura kwa familia nchini Syria wa zinazotaka kufahamu hatma ya jamaa zao wasiojulikana waliko” amesema Guterres.

Guterres ametamatisha ujumbe wake akisema, “ujumbe wangu ni dhahiri: Hatuwezi kuwaangusha wananchi wa Syria. Mapigano lazima yakome. Natoa wito kwa pande zote zishiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa na natoa wito tufanikishe upelekaji wa misaada ya kibinadamu. Lazima tuchague amani.”

Vita nchini Syria ilianza mwezi Machi mwaka 2011 ambapo mwezi Mei mwaka huo huo familia zilianza kukimbia makazi yao kusaka usalama. Wakimbizi wa kwanza waliingia nchini Uturuki.