Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka wa 7 wa vita, bado Syria iko njiapanda- UNHCR

Mwaka wa 7 wa vita, bado Syria iko njiapanda- UNHCR

Wakati dunia inajiandaa kushuhudia vita nchini Syria vikiingia mwaka wa saba tangu vianze, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limetaka jamii ya kimataifa iongeze maradufu usaidizi wake wakati huu ambao mamilioni ya raia wanaendelea kukumbwa na machungu. Grace Kaneiya na taarifa kamili.

(Taarifa ya Grace)

Filippo Grandi ambaye ni Kamishna Mkuu wa UNHCR amesema Syria iko njiapanda na iwapo hakuna hatua thabiti zinachukuliwa kusaka amani na usalama, hali ya kibinadamu itazidi kuwa mbaya wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unahitaji dola bilioni Nane kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya wasyria walio nyumbani na ugenini.

Hivi sasa watu milioni 13 nukta Tano wanahitaji misaada ya kibinadamu Syria, milioni Sita nukta Tatu wakiwa ni wakimbizi wa ndani huku mamia ya maelfu wakiweka rehani maisha yao ili kusaka hifadhi barani Ulaya.

Bwana Grandi amesema kadri machungu yanavyoendelea, usaidizi nao unapungua hivyo ni matumaini yake kuwa mkutano wa mwezi ujao huko Brussels, Ubelgiji kuhusu Syria unaweza kutathmini mustakhbali wa nchi hiyo ikiwemo mahitaji ya kibinadamu.