Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa UN atoa wito kwa wapiganaji kuepuka kuwashambulia raia

Wakimbizi kutoka Ukraine wakivuka mpaka kuingia Medyka, Poland.
© UNICEF/John Stanmeyer VII Photo
Wakimbizi kutoka Ukraine wakivuka mpaka kuingia Medyka, Poland.

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa UN atoa wito kwa wapiganaji kuepuka kuwashambulia raia

Amani na Usalama

Katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika leo Jumatatu jioni katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, kuhusu hali ya Ukraine katika siku ya kumi na mbili ya mashambulizi ya Urusi, Naibu Katibu Mkuu katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Martin Griffiths ametoa wito kwa wapiganaji kuwaepusha raia. 

"Ninaona vipaumbele vitatu vya haraka ili kupunguza uchungu na mateso ambayo sote tunaona yakitokea kwa wakati halisi." Martin Griffiths, amewaeleza wajumbe wa Baraza la Usalama. 

Vipaumbele vitatu 

Bwana Griffiths amesema kwanza pande zote zinazohusika katika mzozo lazima zihakikishe wakati wote zinawaokoa raia na makazi ya raia na miundombinu katika operesheni zao za kijeshi. Hii ni pamoja na kuruhusu kupita kwa usalama kwa raia wanaoondoka kwa hiari katika maeneo yenye uhasama mkali, kwa uelekeo watakaouchagua wao wenyewe na kwamba raia wote iwe wanabaki au wanaenda, lazima waheshimiwe na kulindwa. 

"Pili, tunahitaji njia salama kwa misaada ya kibinadamu katika maeneo yenye mgogoro unaoendelea. Raia katika maeneo kama Mariupol, Kharkiv, Melitopol na kwingineko wanahitaji sana msaada, hasa vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha. Mbinu nyingi zinawezekana, lakini hili lazima lifanyike kwa mujibu wa wahusika chini ya sheria za vita.” Ameeleza. 

Tatu, kwa mujibu wa Martin Griffiths, kuna haja ya haraka ya mfumo wa mawasiliano ya mara kwa mara na wahusika kwenye mzozo na uhakikisho wa kuruhusu utoaji wa misaada ya kibinadamu kwani, "mfumo wa taarifa za kibinadamu unaweza kusaidia utoaji wa misaada kwa kiwango kinachohitajika." 

Aidha Bwana Griffiths ameonesha kuwa tayari ofisi yake imeanza mawasiliano na pande zinazohusika kuhusu mapendekezo hayo akisema, "katika hoja yangu ya tatu, ofisi yangu ilituma timu huko Moscow kufanya kazi katika uratibu bora wa kibinadamu wa kijeshi ambao ungeweza kuturuhusu kuongeza juhudi zetu. Hii inafuatia simu ya Ijumaa iliyopita kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu.”