Kura za maoni katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi haziwezi kuwa halali - UN 

Rosemary DiCarlo, Msaidizi wa Katibu Mkuu UN katika Masuala ya Kisiasa na Kujenga Amani, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Ukraine. Julai, 29, 2022
UN Photo/Mark Garten
Rosemary DiCarlo, Msaidizi wa Katibu Mkuu UN katika Masuala ya Kisiasa na Kujenga Amani, akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Ukraine. Julai, 29, 2022

Kura za maoni katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi haziwezi kuwa halali - UN 

Amani na Usalama

Msaidizi wa Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa na amani Rosemary DiCarlo amewaeleza Jumanne hii wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu kura ya maoni katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na majeshi ya Urusi; akidai kuwa upigaji kura haulingani na “udhihirisho wa kweli wa nia ya watu wengi.” 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili hali ya Ukraine. Bi Rosemary DiCarlo, akiangazia mchakato wa kura za maoni zilizoandaliwa na serikali ya Urusi katika mikoa ya Ukraine inayokaliwa kwa mabavu na Urusi amesisitiza kuwa kura haziendani na matakwa ya walio wengi kwa kuwa zinafanyika wakati wa mapigano ya silaha katika maeneo ambayo yanakaliwa na Urusi  na nje ya utaratibu kikatiba na kisheria ya Ukraine.  

Ukiukaji wa sheria ya kimataifa 

Upigaji kura ulianza Septemba 23 huko Donetsk, Luhansk, Kherson, na Zaporizhzhia. DiCarlo anasema kuwa uchaguzi ulifanyika katika vituo vya kupigia kura na pia watu walifuatwa na mamlaka zinazokalia eneo hilo huku wakiwa wanaambatana na askari katika makazi ya watu. 

Rosemary DiCarlo ameongeza kuwa "vitendo vya upande mmoja vilikusudia kutoa mfano wa uhalali wa jaribio la kunyakua kwa nguvu kwa taifa moja kwa jingine huku vikidai kuwakilisha matakwa ya watu, haviwezi kuchukuliwa kuwa halali chini ya sheria za kimataifa.”   

Msaidizi huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa mfano wa kuongezeka kwa ghasia na milipuko mipya ya mabomu dhidi ya miundombinu ya kiraia. Kwa mujibu wa takwimu, tayari kuna majeruhi raia 14,800 na watu 5,996 wamefariki dunia na 8,848 wamejeruhiwa. 

Vitisho vya nyuklia 

Rosemary DiCarlo ametaja vitisho vya matumizi ya silaha za nyuklia kuwa "havikubaliki" na akasisitiza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kwa mataifa yote yenye silaha za nyuklia, ikiwa ni pamoja na Urusi, kuahidi kutotumia na kuondokana na silaha za nyuklia hatua kwa hatua. 

Pia aameangazia kazi ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na akabainisha kuwa changamoto ya ufikiaji inaendelea katika Donetsk, Luhansk, Kherson, Mykolaiv na Zaporizhzhia, ambazo ziko nje ya udhibiti wa Ukraine. 

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na siasa, kuna ripoti za kutisha za ukiukaji wa haki za binadamu. Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inachunguza madai katika maeneo ya eneo la Kharkiv, ambayo hadi hivi majuzi yalikuwa chini ya udhibiti wa Urusi. 

Aidha DiCarlo amebainisha kuwa baada ya uatafiti katika maeneo ya Kyiv, Chernihiv, Kharkiv na Sumy, Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Ukraine ilihitimisha kuwa uhalifu wa kivita umetendwa nchini humo. 

Pia ameangazia kazi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, AIEA, huko Zaporizhzhia na kuzitaka pande zote husika kushirikiana kuendesha kazi hiyo na vile vile kuanzisha tena udhibiti wa raia kwa mtambo huo. 

Janga la njaa 

Mwisho, DiCarlo ametoa mfano wa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao unapaswa kufanywa upya mnamo Novemba ili kuepuka janga la chakula duniani. 

Kwa mujibu wa DiCarlo juhudi za kuondoa vizuizi vya usafirishaji wa pembejeo za Urusi zinaendelea na kwamba bidhaa hizi haziko chini ya vikwazo na lazima zifikie masoko ya dunia. 

Aidha amesema makubaliano hayo tayari yamesafirisha zaidi ya tani milioni 4.5 za chakula katika Pembe ya Afrika, Yemen na Afghanistan. 

Rais wa Ukraine 

Kikao hicho kimehudhuriwa na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kwa njia ya mtandao.  

Katika hotuba yake, ametoa wito wa 'dhamana ya pamoja' kwa usalama wa Ukraine, kwa ajili ya kutengwa kwa Urusi, pamoja na kuondolewa kwa kura ya turufu katika Baraza la Usalama na kupigwa marufuku kwa taifa hilo katika taasisi nyingine za kimataifa. 

Wanachama wengine wa Baraza la Usalama pia wamesema kwamba hawatambui uhalali wa kura za maoni.