Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polio yabainika Malawi, WHO yachukua hatua 

Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio
WHO
Kampeni ya utoaji chanjo ya Polio

Polio yabainika Malawi, WHO yachukua hatua 

Afya

 Malawi imetangaza kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa polio nchini humo na hivyo kuwa ni tangazo la kwanza la uwepo wa ugonjwa huo barani Afrika katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika iliyotolewa leo jijini Brazaville Congo na Lilongwe Malawi imesema tangazo hilo linafuatia kubainika kwa mtoto mdogo mwenye ugonjwa huo kwenye mji mkuu Lilongwe. 

Kufuatia hatua ya mamlaka za Malawi kutoa taarifa hizo, WHO kanda ya Afrika imesema inachukua hatua zote kudhibiti kusambaa kwa Polio na huku ikisema kuwepo kwa mikakati bora ya ufuatiliaji ndio kumewezesha kubainika kwa mgonjwa huyo. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema uchambuzi wa kimaabara umebainisha kuwa Polio hiyo iliyogundulika Malawi ni kama ile iliyojikita jimbo la Sindh nchini Pakistani. 

“Kwa kuwa aina hii iliyobainika ni kutoka Pakistani, kwa hiyo haitoathiri hadhi ya Afrika ya kuthibitishwa kuwa haina Polio,” amesema Dkt. Moeti. 

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio huko Cotonou nchini Benin
©Yézaël Adoukonou/ Nations Unies Bénin
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio huko Cotonou nchini Benin

Kadri polio hii inaendelea kuweko kokote kule, nchi zote zinakuwa hatarini kupata virusi hivi, amesema Dkt. Moeti akiongeza kuwa hivi sasa wanasaidiana na mamlaka za afya za Malawi kutathmini hatari ya kubainika kwa mgonjwa huyo mmoja ikiwemo kutoa chanjo za ziada, ufuatiliaji hata katika nchi Jirani. 

Mpango wa kutokomeza polio duniani, GPEI wenye makao yake Brazaville, Congo unatuma timu yake kusaidia uratibu, ufuatiliaji, na usimamizi wa takwimu pamoja na mawasiliano ya kudhibiti kusambaa kwa Polio Malawi. 

Mgonjwa wa mwisho wa Polio aina hii iliyobainika Malawi, alipatikana kaskazini mwa Nigeria mwaka 2016 na duniani kote hadi mwaka jana wa 2021 kulikuweko na wagonjwa watano pekee 

Polio ni ugonjwa hatari unaoambukiza ambao unasababishwa na virusi. Virusi hivyo hushambulia mfumo wa fahamu na vinaweza kusababisha mgonjwa kupooza katika saa chache. 

Usambazaji wake kutoka kwa mtu hadi kwa mwingine ni kupitia choo, chakula na ingawa hakuna tiba ya Polio, ugonjwa huo unazuilika kwa chanjo.