Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yataja nchi zitakazozalisha chanjo za kwanza za mRNA barani Afrika 

Maabara kwenye kituo cha kuhamisha teknolojia ya mRNA nchini Afrika Kusini moja ya nchi ambazo zimechaguliwa kuanzisha uzalishaji wa chanjo ya mRNA
MPP/WHO/Rodger Bosch
Maabara kwenye kituo cha kuhamisha teknolojia ya mRNA nchini Afrika Kusini moja ya nchi ambazo zimechaguliwa kuanzisha uzalishaji wa chanjo ya mRNA

WHO yataja nchi zitakazozalisha chanjo za kwanza za mRNA barani Afrika 

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO leo limezitaja nchi za Misri, Kenya, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia kuwa zitakuwa nchi za kwanza katika bara la Afrika kupokea teknolojia inayohitajika kuzalisha chanjo za mRNA, ambazo zimeonekana kuwa muhimu katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19. 

Tangazo hilo limetolewa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo mjini Geneva Uswis katika hafla iliyoandaliwa na WHO, Baraza la Ulaya, serikali za Ufaransa na Afrika Kusini na marais husika wa kila mmoja kuhudhuria. 

"Hakuna tukio lingine kama janga la COVID-19 ambalo limeonyesha kuwa kutegemea kampuni chache kusambaza bidhaa zinazohitajika kwa umma ulimwenguni ni changamoto na ni hatari," amesema mkurugenzi huyo mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus. 

Ameongeza kuwa teknolojia inayoleta mapinduzi ya mRNA hufundisha seli za mwili jinsi ya kutengeneza protini ambayo huchochea mwitikio wa kinga, bila kutumia nyenzo yoyote ya virusi. Kati janga la COVID-19, inaongeza uzalishaji usio na madhara wa protini ikiutahadharisha mwili kujikinga na virusi. 

Uzalishaji wa chanjo nyumbani 

Wanawake mafundi wanaofanyakazi katika kituo cha kuhamisha teknolojia cha mRNA nchini Afrika Kusini
MPP/WHO/Rodger Bosch
Wanawake mafundi wanaofanyakazi katika kituo cha kuhamisha teknolojia cha mRNA nchini Afrika Kusini

Kituo cha kimataifa cha uhamishaji wa teknolojia cha mRNA kilianzishwa nchini Afrika Kusini mwaka jana ili kusaidia nchi za kipato cha chini na cha kati katika kutengeneza chanjo zao za mRNA kwa taratibu za uendeshaji zinazohitajika na ujuzi wa kufikia viwango vya kimataifa. 

Ingawa kimeundwa kushughulikia dharura ya janga la COVID-19, lakini kituo hicho kina uwezo wa kupanua wigo wake na kutengeneza dawa zingine, na kuziweka nchi katika usukani linapokuja suala la aina za chanjo zinazohitajika kushughulikia vipaumbele vyao vya afya. 

Kulingana na miundombinu ya nchi, nguvu kazi na uwezo wa udhibiti, WHO na washirika watafanya kazi nao kutengeneza muongozo, kuandaa mafunzo na kutoa usaidizi ili kuanza kutoa chanjo zenye ufanisi zaidi nyumbani, haraka iwezekanavyo. 

"Huu ni mpango ambao utaturuhusu kutengeneza chanjo zetu wenyewe na hiyo inamaanisha kuwepo na kuheshimiana, kuwekeza katika uchumi wetu na, kwa njia nyingi, kurejesha fadhila kwa bara letu", amesema Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa. 

Mkurugenzi mkuu wa WHo Dkt. Tedros Ghebreyesus na waziri wa maendeleo wa Ubeligiji Meryame Kitir  walipozuru Biovac kituo cha chanjo cha WHo mjini Cape Town Afrika Kusini
WHO/MPP/Rodger Bosch
Mkurugenzi mkuu wa WHo Dkt. Tedros Ghebreyesus na waziri wa maendeleo wa Ubeligiji Meryame Kitir walipozuru Biovac kituo cha chanjo cha WHo mjini Cape Town Afrika Kusini

Kitovu cha utengenezaji  

 Ili kuhakikisha kuwa kila nchi inajenga uwezo wa kuzalisha chanjo na teknolojia zao za afya, WHO imekuwa ikianzisha kituo cha mafunzo ya wafanyakazi wa kutengeneza dawa mbalimbali kwa mataifa yanayovutiwa na uzalishaji na utafiti wa kisayansi na kimatibabu, ambayo yatatangazwa katika wiki zijazo. 

Zaidi ya hayo, shughuli za sasa za WHO katika kuunga mkono nchi za kipato cha chini na cha kati zitapanuka kupitia chombo cha kimataifa kinachotathmini uwezo wa nchi kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za afya. 

Pia itatoa mafunzo ya kujenga mifumo imara ya udhibiti na inayofaa kwa madhumuni yanayohitajika. 

"Kwa muda mfupi na muda mrefu njia bora ya kushughulikia dharura za afya na kufikia huduma ya afya kwa wote ni kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kanda zote kutengeneza bidhaa za afya wanazohitaji, na zenye usawa katika upatikanaji ikiwa ndilo lengo lao la msingi," amesisitiza Tedros. 

Uhamishaji wa teknolojia 

 Kituo cha uhamishaji wa teknolojia cha WHO mRNA ni sehemu ya juhudi kubwa zaidi za kuziwezesha nchi za kipato cha chini na cha kati kuzalisha chanjo, dawa na uchunguzi wao wenyewe ili kufikia huduma ya afya kwa wote. 

Juhudi za awali zimejikita katika teknolojia na biolojia ya mRNA, ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa chanjo na inaweza pia kutumika kwa bidhaa zingine, kama vile insulini za kutibu ugonjwa wa kisukari, dawa za saratani na, ikiwezekana, chanjo za magonjwa mengine yanayopewa kipaumbele kama vile malaria, kifua kikuu na VVU. 

Lengo kuu ni kupanua wigo wa uwezo wa uzalishaji wa kitaifa na kikanda kwa teknolojia zote za afya. 

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kuwa katika dunia iliyounganishwa, ushirikiano mpya wenye nguvu kati ya nchi, washirika wa maendeleo na wengine ni muhimu "kuwezesha kanda na nchi kujilinda, wakati wa migogoro, na wakati wa amani". 

Ameongeza kuwa "Faida ya afya ya umma iliyoboreshwa, kusaidia mamlaka ya afya ya Afrika na maendeleo ya kiuchumi ni malengo makuu ya kuimarisha uzalishaji wa ndani barani Afrika".