Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubunifu wa UNICEF Malawi kusambaza chanjo ya Covid-19 mtaa kwa mtaa wazaa matunda

Wanawake wakiwa wamejipanga mstari ili kupata chanjo dhidi ya Covid-19 nchini Malawi.
© UNICEF/ Thoko Chikondi
Wanawake wakiwa wamejipanga mstari ili kupata chanjo dhidi ya Covid-19 nchini Malawi.

Ubunifu wa UNICEF Malawi kusambaza chanjo ya Covid-19 mtaa kwa mtaa wazaa matunda

Afya

Mnyumbuliko wa hivi karibuni wa virusi vya Corona vinavyosababisha Covid-19, Omicron ukiwa umesambaa ulimwenguni kote, ukosefu wa usawa wa chanjo unaweka baadhi ya watu hatarini zaidi kuruhusu minyumbuliko kubadilika na kuathiri wanadamu wengine. Afrika ina idadi ya chini zaidi ya watu waliochanjwa dhidi ya COVID-19 duniani lakini nchini Malawi mradi bunifu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wa kusambaza chanjo kwa njia ya gari unaongeza upatikanaji wa chanjo na imani ya chanjo miongoni mwa wanawake wajawazito katika jamii za vijijini.

Albert Dzikolatha ambaye ni Bwana Afya, anasema hivi karibuni wamepokea mchango wa gari la chanjo ya haraka, ambalo wanaweza kutumia kupeleka chanjo kwenye jamii ambazo ni vigumu kuzifikia, na watu wanapata chanjo hapo hapo. 

Eliza Sophas ni mjamzito anasema, "ni muhimu kuwa na gari linalokuja kwetu na kutupa taarifa, kwa sababu kijiji chetu kiko mbali sana na hospitali ya karibu hasa kwa sisi wajawazito, ni mbali sana. Kwa hivyo, gari linapokuja tunapata habari na huduma haraka. 

Gari wanaloliongelea ni Basi dogo au kama waitavyo wengine, Min-Bus au Van. Juu limebeba spika mbili kubwa kwa ajili ya kupaza sauti za matangazo kuhusu chanjo. Mradi huu tayari unazaa matunda. Ness Kapondera ni Mkunga Muuguzi anathibitisha matunda mazuri ya ubunifu huu wa UNICEF akisema, "Tunapolinganisha takwimu zetu za chanjo za kila siku, tunapochanja hapa hospitalini na idadi tunapochanja huko mitaani. Tunachanja watu wengi zaidi nje kwa kuwa tunatembea hap ana pale na kutumia gari la haraka. Tunachanja watu wengi zaidi sasa kuliko hapo awali."