Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 116 kuzaliwa miezi 9 baada ya COVID-19 kutangazwa janga, je changamoto ni zipi?

Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha
UNFPA Mozambique
Mkunga Adelaide Raul kutoka Msumbiji akifurahi na mama baada ya kumzalisha watoto mapacha

Watoto milioni 116 kuzaliwa miezi 9 baada ya COVID-19 kutangazwa janga, je changamoto ni zipi?

Afya

Kuelekea siku ya mama duniani tarehe 10 mwezi huu wa Oktoba, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linakadiria kuwa watoto milioni 116 watakuwa wamezaliwa wiki 40 tangu ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 utangazwe kuwa janga la kimataifa tarehe 11 mwezi Machi mwaka huu.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema kuwa, “wanawake waliojifungua na watoto watachanga watakumbana na machungu mapya ikiwemo hatua za kuzuia kuchangamana, vituo vya afya kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma, ukosefu wa vifaa vya matibabu, uhaba wa wahudumu wa afya wenye stadi za kutosha kwa kuwa wengi wanahudumia wagonjwa wa Corona sambamba na amri za kutotembea hovyo.”

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema kuwa mamilioni ya wazazi duniani kote wanaanza safari ya uzazi kama ilivyokuwa akisema kuwa, "wanalazimika kujiandaa kuleta kiumbe duniani katika dunia ambayo kwayo, wajawazito wanahofia kwenda vituo vya afya kwa hofu ya maambukizi, au wanakosa huduma ya dharura kutokana na vituo vya afya kuzidiwa uwezo au kutokana na amri ya kutotembea hovyo.”

Bi. Fore amesema ni vigumu sana kufikiria ni kwa jinsi gani gonjwa la Corona limeathiri uzazi na hivyo UNICEF inaonya kuwa, “hatua za kuzuia watu kutoka majumbani mwao zinaweza kuvuruga huduma za afya za kuokoa maisha kama vile huduma za kujifungua na hivyo kuwaweka mamilioni ya wajawazito na watoto wao hatarini.”

Daktari akimchunguza mjamzito kwenye kituo cha afya cha Gbaleka, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.
© UNICEF/UNI326749// Frank Dejongh
Daktari akimchunguza mjamzito kwenye kituo cha afya cha Gbaleka, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.

Je ni nchi zipi zitakuwa na watoto wengi zaidi?

UNICEF inasema kuwa nchi zinazotarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watoto miezi 9 baada ya COVID-19 kutambuliwa kuwa ni janga ni pamoja na India watoto milioni 20.1, China, watoto milioni 13.5, Nigeria watoto milioni 6.4 huku Pakistan ikitarajia watoto milioni 5 na Indonesia watoto milioni 4.

Shirika hilo linasema kuwa idadi kubwa ya mataifa hayo tayari yana viwango vya juu vya vifo vya watoto wachanga, hata kabla ya janga la COVID-19 na hivyo viwango hivyo vinaweza kuongezeka wakati huu wa Corona.

Marekani nayo ambayo imeathiriwa na janga la Corona inatarajia zaidi ya watoto milioni 3.3 kuzaliwa kati ya Machi 11 hadi Desemba ambapo mamlaka za jimbo la New York, zinaangalia mbinu ya kuweka vituo vya kujifungulia kwa kuwa wajawazito wengi wanahofia kwenda kujifungulia hospitalini.
 
UNICEF inaonya kuwa ingawa ushahidi unaonesha kuwa wajawazito hawaathiriwi zaidi na COVID-19 kama ilivoy kwa watu wengine, serikali zinapaswa kuhakikisha kuwa bado wanapata huduma za kabla ya kujifungua, za kujifungua na baada ya kujifungua.

“Vivyo hivyo watoto wachanga wanahitaji huduma za dharura . Familia mpya zinahitaji msaada kuanza kunyonyesha watoto na kupata dawa, chanjo na lishe ili watoto wao wawe na afya,” imesema UNICEF.
 

Ni kwa mantiki hiyo, UNICEF inatoa wito kwa serikali na wahudumu wa afya kuokoa maisha katika miezi ijayo kwa kuchukua hatua ikiwemo, kusaidia wajawazito kupata huduma za uchunguzi kabla, wakati na baada ya kujifungua na huduma zitolewe na wahudumu wenye ujuzi.

Pili, “kuhakikisha wahudumu wa afya wana vifaa vya kujikinga na wanapatiwa kipaumbele katika kupima iwapo wana virusi vya Corona au la na pia iwapo chanjo dhidi ya Corona ikipatikana, wawe wa kwanza kupatiwa ili waweze kutoa huduma bora.”

UNICEF inataka pia kuwepo kwa hakikisho la mbinu za kukinga na kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kwenye vituo vya afya wakati wa kujifungua na baada ya hapo na pia kuwezesha wahudumu wa afya kutembelea wajawazito na wazazi majumbani mwao bila kusahau kutumia teknolojia kama vile simu kufikia wazazi walio maeneo ya ndani zaidi.
 
Ijapokuwa bado haijafahamika iwapo virusi vya Corona vinaweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujautizo, UNICEF inasihi wajawazito wachukue hatua kujikinga na kufuatilia dalili za virusi hivyo.