Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ni ‘mwiba’ kwa wakimbizi na raia nchini Lebanon- UNHCR 

Mkimbizi na mjane wa Syria Majida Shehada Ibrahim, mama wa watoto wanne, akiwasaidia wawili wa binti zake katika masomo yao katika kambi ya Askar huko Lebanon.
© UNHCR/Haidar Darwish
Mkimbizi na mjane wa Syria Majida Shehada Ibrahim, mama wa watoto wanne, akiwasaidia wawili wa binti zake katika masomo yao katika kambi ya Askar huko Lebanon.

COVID-19 ni ‘mwiba’ kwa wakimbizi na raia nchini Lebanon- UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Lebanon, athari za kiuchumi zinazosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, zinaacha raia wa Lebanon pamoja na wakimbizi kutoka Syria wakihaka kujikimu huku baridi kali nayo na njaa vikikosa majawabu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linasema, mwaka huu wa 2022, hali ni tete zaidi kwa kuwa Lebanon nayo nyenyewe imetwama kwenye janga la kiuchumi, hali iliyosababisha na wakimbizi nao kuwa katika hali ya umaskini uliokithiri. 

Miongoni mwa wakimbizi hao ni Majida ambaye ni mjane lakini sasa amesalia na watoto wake anasema, “nina hofu sana na jinsi ya kupata joto hapa. Baridi kali inapoanza nina hofu jinsi ya kutafuta kuni, chakula na nguo. Kila kitu ni gharama. Machungu yalianza tangu mwezi Oktoba. Kambi yetu ilifurika, ni kweli tuna paa lakini limeharibika. Sakafu nayo imefurika, wanangu walilala kwenye sakafu iliyolowana. Hatuna jawabu kwa kuwa hema ni fupi mno.” 

Baada ya kukimbia Syria mwaka 2014 kufuatia mzozo wa zaidi ya muongo mmoja na kifo cha mume wake, Majida na wanawe wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi ya Bekaa, nchini Lebanon na kuna wakati anapata kibarua shambani huku watoto wake wawili wakubwa wa kiume wakifanya kazi za vibarua shambani kwa kuwa ilibidi waache shule familia iweze kujikimu, “matamanio yangu ni Lebanon, nchi ambayo imekuwa karimu kwangu, hali yake ya amani iimarike kwa sababu hali ni ngumu kwa kila mtu, iwe walebanon au wakimbizi.” 

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, UNHCR imepatia usaid​izi wa marekebisho ya makazi kwa familia za walebanon na wakimbizi pamoja na taa za sola na vifaa muhimu vya familia hasa wakati huu wa majira ya baridi kali.