Maisha mapya Hispania ni kutimiza ndoto yangu na familia yangu:Mkimbizi Ghaith 

19 Oktoba 2020

Kutana na mtoto mkimbizi kutoka Syria na familia yake wanaoishi nchini Lebanon, ambao mpango wa shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wa kuwapeleka wakimbizi nchi ya tatu unawapa fursa ya kwenda kuishi Hispania, hatua wanaiona ni mwanya wa kutimiza ndoto ya muda mrefu. Kulikoni?

Huyo ni Gaithi Mohammed mtoto wa miaka 13 mkimbizi kutoka nchini Syria akisema anaenda Hispania kusakata kabumbu.
Ghaith na familia yake walikimbia vita Syria baada ya kupata vitisho vya kuaawa na kwenda kupata hifadhi Lebanon. 

Ndoto yake ni siku moja kuwa mchezaji wa kandanda kwenye timu ya Real Madrid. Ghaith hawezi kusoma kwa sababu analazimika kufanyakazi kumisaidia baba yake aitwaye Samer Mohammed ambaye anasema,“Nina matatizo ya kiafya hivyo watoto wangu wawili hawa wakubwa wananisaidia kusukuma mkokoteni wa mbogamboga ninazouza. Wanapandisha kwenye majengo hadi ghorofa ya 6 au ya 7 bila lifti, wanafanyakazi kwa bidi sana pamoja nami.” 

Mohammed anasema maisha yao kila siku ni ya kubambanya ili kuweza kuishi,“Leo tunaweza kuwa na chakula na kesho tukakosa, kwa vyovyote vile ni lazima tulipe kodi ya pango” 

Baada ya dhiki kweli ni faraja, sasa UNHCR inaihamishia familia nzima katika nchi ya tatu Hispania, furaha ya Mohammed haifichiki ,“Ni kama tunazaliwa upya, ninataka kuleta watoto wangu upya kabisa” 

Kwa mujibu wa UNHCR duniani kote wakimbizi wanaohitaji kupelekwa nchi ya tatu ni wengi lakini wanaofanikiwa ni chini ya asilimia 7. Lakini kwa Gaithi na famialia yake ni ndoto iliyotimia japo Mohammed anasema mwanaye Gaith,“Bado anaota kuzuru uwanja wa Real Madrid na kupiga picha na Benzema. Nilikuwa namwambia haiwezekani sisi kwenda huko lakini sasa ndiko tunakoelekea.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud