Vita Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini vyawabebesha watoto gharama:UNICEF

5 Februari 2018

Vita na ghasia zilizotamalaki Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini hususani kwa mwezi wa Januria zimewabebesha gharama kubwa watoto, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Tupate taarufa Zaidi na John Kibego.

Kwa mujibu wa Geert Cappelaere mkurugenzi wa Kanda hiyo wa UNICEF, watoto wengi wameuawa katika vita, mashambulizi ya kujitolea muhanga au wamepigwa na baridi hadi kufa wakijaribu kukimbia maeneo hayo yaloghubukwa na machafuko.

Amesema hali hiyo haikubaliki kwa watoto kupoteza maisha yao na kujeruhiwa  kila uchao, akitolea mfano Iraq, Libya, Palestina, Syria na Yemen ambako Januari pekee watoto 83 wamepoteza Maisha.

Ameongeza kuwa watoto hao wamelipa gharama kubwa ya vita wasivyo na wajibu navyo na kuwaacha wazazi na familia zao na simanzi ya daima.

Huko Syria mapigano yaliyoshika kasi katika wiki nne zilizopita yamearifiwa kukatili Maisha ya watoto 59, wakati Yemeni watoto 16 maisha yao yamekatishwa pasi sababu na Lebanon watu 16 wakiwemo watoto wanne walipigwa baridi hadi kufa wakikimbia vita Syria.

Sio mamia, wala maelfu amesema Cappelaere, bali ni mamilioni ya watoto katika kanda hiyo ambao utoto wao umeporwa , wamesalia vilema wa kimwili na kisaikolojia, huku wengine wakiendelea kunyanyaswa, kuwekwa rumande, kukosa elimu na huduma muhimu za afya.

Amesisitiza kuwa ingawa watoto hao wamenyamazishwa kwa sasa, lakini sauti zao zitaendelea kusikika na ujumbe wao ni huu"ulinzi kwa watoto ni lazima katika mazingira yoyote yale kwa mujibu wa sheria za vita", na kukiuka sheria hizo ni uhalifu mkubwa unaoweka njia panda , mustakhbali sio tu wa watoto bali wa mataifa hayo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud