Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majira ya baridi yameanza Lebanon wakimbizi wahaha huku ukata ukizidisha adha:UNHCR 

Mtoto mkimbizi kutoka Syria akiwa kwenye makazi ya muda nchini Lebanon.
UNICEF/ Dar Al Mussawir
Mtoto mkimbizi kutoka Syria akiwa kwenye makazi ya muda nchini Lebanon.

Majira ya baridi yameanza Lebanon wakimbizi wahaha huku ukata ukizidisha adha:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Maelfu ya wakimbizi nchini Lebanon sasa wanaanza kuhaha kwani majira ya baridi yamewadia na kila mwaka huwapa changamoto kubwa lakini mwaka huu madhila yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mgogoro wa kiuchumi na mfumoko wa bei ulioanza Oktoba mwaka 2019 ambao sasa umefikia asilimia 174. Yote haya yanamanisha fedha na msaada wanaopewa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR hautokidhi mahitaji.

Huyu ni mkimbizi Huda kutoka Syria anayeishi kwenye kambi ya bonde la Bekaa, kama walivyo wakimbizi wengine anahofia sana msimu wa baridi na fedha kidogo alizokuwa nazo tayari amenunulia gesi ili apashe joto hema lake akisema asipofanya hivyo basi watoto wake wataugua na itambidi kutumia fedha kununua dawa na kisha kumlazimu kukopa tena fedha na hivyo kuishi na madeni. 

Na changamoto hii si ya Huda peke yake bali ya maelfu ya wakimbizi katika makazi haya ya Bekaa. Siham al-Jassim ni mama anayelea wanawe peke yake anasema,“Wanangu waliniomba niwanunulie nguo za baridi akini siwezi kumudu kununua. Vitu ni ghali sana na msimu wa baridi umeshafika. Cha kwanza  kwangu ni kuhakikisha tuna gesi ya kupasha joto hema.” 

Shirika la UNHCR linazisaidia familia hizi za wakimbizi kwa kuwapa fedha,  nguo, vifurushi vya chakula na gesi sababu linatambua hali halisi kama anavyosema msemaji wa shirika hilo Dalal Harb,“Usiache jua  hili linaloonekana likakudanganya, majira ya baridi yamewadia, na safari hii kwa wasiojiweza na wale ambao tayari walikuwa wameathirika na kuporomoka kwa uchumi, janga la COVID-19 na mlipuko wa Beiruti ,watakabiliwa na madhila zaidi katika miezi minne ijayo ambapo msimu wa baridi kali utakaposhika kasi. Na msimu huu haubagui, hauchagui uwe Mlebanon au mkimbizi”. 

Msaada wa fedha kwa wakimbizi kama Huda utawasaidia kuhakikisha wanakuwa salama msimu huu wa baridi

Nattss….. na anasema msaada huo ni baraka kubwa kwake. 

Na kwa Siham ombi la wanawe limetimia , kwani leo ammepokea msaada wa nguo mpya kutoka UNHCR

“Watoto wamefurahi sana kupata nguo hizi, na furaha yao imeongezeka zaidi sababu wamepata kitu kipya." 

UNHCR inasema katika majira haya ya baridi  itahakikisha maelfu ya wakimbizi na pia raia wa Lebanon wanapata msaada katika miezi ijayo ili kuwavusha msimu huu mgumu.