Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 1.5 wako hatarini Pembe ya Afrika, zaidi ya dola milioni 138 zahitajika

Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka
FAO/IFAD/WFP/Michael Tewelde
Ukame nchini Somalia unasababisha njaa kuongezeka na viwango vya utapiamlo kuongezeka

Watu milioni 1.5 wako hatarini Pembe ya Afrika, zaidi ya dola milioni 138 zahitajika

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya dola milioni 138 za ufadhili wa dharura zinahitajika kusaidia watu milioni 1.5 walio hatarini katika jamii za vijijini katika Pembe ya Afrika ambao mashamba yao  na malisho ya mifugo yameathiriwa na ukame wa muda mrefu.

Hayo yamesemwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo -FAO hii leo jijini Roma nchini Italia wakati wakitoa ripoti ya kina kuhusu mpango wa kukabiliana na changamoto za kilimo na aina ya msaada unaoitajika kwa kila kanda.

Pembe ya Afrika ni eneo ambalo tayari linakabiliwa na uhaba wa chakula unaohusishwa na hali mbaya ya hewa, vikwazo vya maliasili na migogoro, janga la COVID-19 na uvamizi wa nzige wa 2020-2021 ambao umefanya jamii kukabiliana na changamoto hizi hadi kufikia ukomo kudhoofisha uzalishaji wa kilimo.

Nchi za Ethiopia, Kenya na Somalia, ndio zilizoathirika zaidi, makadirio yanaonesha kuwa takriban watu milioni 25.3 watakuwa hawana uhakika wa chakula ifikapo katikati ya mwaka wa 2022. Na ikiwa usaidizi hautapatikana na hali hiyo itatokea basi Pembe ya Afrika itakuwa kati ya nchi zinazokabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula duniani.