Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 7 zinahitaji kusaidia pembe ya Afrika

Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu
UNICEF/Raphael Pouget
Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu

Dola bilioni 7 zinahitaji kusaidia pembe ya Afrika

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo jijini New York Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwakushirikiana na nchi saba wanachama wa UN wanaendesha tukio la uchangishaji fedha lengo likiwa ni kukusanya dola bilioni 7 kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu kwa nchi zilizopo pembe ya Afrika.

Kwa miongo kadhaa pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na ukame mkali hali iliyofanya takriban watu milioni 43.3 kuhitaji usaidizi wa kuokoa maisha na kustahimili changamoto zinazo wakabali hususan katika nchi za Kenya, Somalia na Ethiopia.

Ukame umeleta njaa, kutokuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula na shida ya maji ambayo inachangia katika kuleta magonjwa.

Hivi karibuni mvua zimeanza kunyesha, wananchi wamekuwa wakitarajia zitasaidia kupunguza changamoto zao lakini kama waswahili wasemavyo ‘ngombe wa masikini hazai’ ndicho kilichotokea kwa nchi hizo kwani mvua kubwa zimeleta mafuriko na kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA zaidi ya watu 900,000 wameathiriwa na mvua hizo.

Mmoja wa watu hao ni Abdirahaman Ali Sheikh kutoka nchini Somalia, "Angalia hali ilivyo sasa, maji yametapakaa kwenye nyumba yangu yote na watoto wangu.”

Bi. Qiyaas Axmed Farax amelazimika kuyakimbia makazi yake sababu ya mafuriko na sasa anahitaji msaada wa kibinadamu, “Tunahitaji chakula, malazi na maji, hatuna kitu, nguo zetu, vyakula na vingine vyote vimesombwa na maji. Watoto wangu walikuwa hatarini lakini namshukuru Mungu kwasasa tupo salama.”

Mkutano huu wa ngazi za juu unaofanyika hapa jijini New York Marekani unatarajia kusaidia zaidi ya watu milioni 32 ikiwemo hawa waliathirika na mafuriko.

Nchi saba zinazoshirikiana na Katibu Mkuu Guterres katika kendesha tukio hilo la ahadi ni Marekani, Uingereza, Qatar, Italia pamoja na nchi ambazo zinauhitaji wa haraka wa misaada hiyo ambazo ni Ethiopia, Somalia na Kenya.