Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa Colombia, Guterres ajionea maendeleo na changamoto za mkataba wa amani 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres akizungumza na wanavijiji mjini Llino Grande nchini Colombia ambako amejionea jinsi mchakato wa amnai unasonga mbele.
UNMVC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na wanavijiji mjini Llino Grande nchini Colombia ambako amejionea jinsi mchakato wa amnai unasonga mbele.

Akiwa Colombia, Guterres ajionea maendeleo na changamoto za mkataba wa amani 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko ziarani nchini Colombia, amejionea maendeleo na changamoto za mkataba wa amani uliofikiwa nchini humo miaka mitano iliyopita kati ya serikali na wapiganaji wa zamani wa kikundi cha FARC.

Mkataba wa amani Colombia ulipitishwa mwezi Novemba mwaka 2016. Akiwa nchini humo hii leo jumanne ametembelea mji wa Llano Grande, ulioko jimbo la Antioquia akiwa ameambatana na Rais Ivan Duque wa Colombia na kamanda wa zamani wa kikundi cha FARC-EP  Rodrigo Londoño. 

Guterres amesema mji huo ni saw ana ‘maabara ya amani’ ambako suala la wapiganaji wa zamani kutangamana katika maisha ya kiraia kwenye jamii liko bayana  sambamba na changamoto ambazo zinaibuka.

Colombia ina majimbo 32  ambapo Antioqua ni moja ya majimbo yaliyoathirika vibaya na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka 50 na asilimia 80 ya wakazi wake walidhuriwa na mapigano hayo.

Mji wa Llano Grande wenye wakazi 150, ambako wale waliokuwa maadui zamani sasa wanaishi pamoja na jamii na kufanya kazi pamoja.

Kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na serikali, kijiji kimoja kidogo kimekuwa pahala ambapo aman imetawala kiasi kwamba wapiganaji wa zamani wa FARC na wenyeji wanajiona ni familia moja.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitembelea karakana ya ushoni inayotangamanisha wapiganaji wa zamnai na raia huko Llano Grande nchini Colombia
UNMVC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitembelea karakana ya ushoni inayotangamanisha wapiganaji wa zamnai na raia huko Llano Grande nchini Colombia

 

Katibu Mkuu alitembelea kwenye mji huo katika mazingira ya kawaida kabisa na kuweza kuzungumza na wakazi hao ambao wananufaika na miradi mbalimbali ya ujasiriamali.

“Nimefurahi sana kuwa hapa Llano Grande na kujionea mwenyewe mafanikio ya amani,” amesema Katibu Mkuu wakati akitembelea karakana ya mradi wa ushoni.

Akiwa kwenye karakana hiyo amezungumza na mfanyakazi Monica Astrid Oquendo ambaye hivi karibuni aliieleza Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa Mkataba wa amani umeleta mipango ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii.

Guterres alizungumza pia na wafanyakazi wengine kuhusu kazi zao na kujadili umuhimu wa wanawake kushika hatamu ya uongozi katika mchakato wa amani.

Aina mpya ya kahawa

Wakati huo huo, kundi la wapiganaji wa zamani wametumia ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuzindua “Trópicos, aina mpya ya kahawa iliyobuniwa na ushirika wenye wanachama 1200.

Guterres alivutiwa sana mchakato wa kilimo cha mmea uzalishao kahawa hiyo aina ya Trópicos sambamba na aina nyingine za buni nchini Colombia.

Kwa lugha ya kispanyola. “Trópicos  ni eneo la kitropiki na aina hiyo ya kahawa inalimwa kwenye maeneo ya tabianchi ya kitropiki.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na wanavijiji wa Llano Grande ambako amejionea maendeleo ya mchakato wa amani nchini Colombia
UNMVC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na wanavijiji wa Llano Grande ambako amejionea maendeleo ya mchakato wa amani nchini Colombia

Aina hiyo ya kahawa ni ya kipekee kutokana na eneo inakolimwa na wakulima wenyewe walio katika mchakato wa utangamano.

Mmoja wa wabunifu wa kahawa hiyo Frey Gustavo de Mate amesema Trópicos  siyo tu ina historia ya kijamii bali pia viwango vyake ya ubora kwa kuwa “tumechagua kahawa bora kabisa ili kupata iliyo bora na tunasema kutoka kwenye eneo la kitropiki kwenda duniani.”

Katibu Mkuu ameelezwa pia kuhusu miradi mingine kama vile shule, duka la kuoka mikati ya kikolombia na kiwanda cha sabuni.

Baadaye akizungumza na wanajamii kwenye uwanja wa soka, Katibu Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza kila mmoja kwa ari na kujitoa kwao katika miradi hiyo ambayo inaungwa mkono na serikali na jumuiya ya kimataifa.

Amani haiji siku moja

Baada ya kusikiliza maoni ya wanajamii, Guterres aliwaeleza kuwa wananchi hao ndio wanaotambua fika kuliko watu wengine ya kwamba amani haiji kwa siku moja.

“Ina gharama zake kuijenga, kuilea na kuiendeleza. Kuna utata katika lengo la amani kwamba ni jamii bila maadui, lakini kwa bahati mbaya bado kuna maadui wa amani.” Amesema Guterres huku akionesha mshikamano na manusura na familia zao.

Tangu mwaka 2017, kumekuweko na matukio 30 ya mauaji na matukio 4 ya watu kutoweka, wengi wao wanaume na wote hao ni katika mkoa wa Antioquia.
Nchini Colombia kwa ujumla kumekuweko na matukio 303 ya mauaji ya wapiganaji wa zamani na wengine 25 wametoweka. Takribani watetezi 500 wa haki za binadamu na viongozi wa kijamii nao wameuawa katika mashambulio.

Hata hivyo Guterres amevutiwa na azma ya watu wa eneo hilo ya kuendelea kujenga amani nchini Colombia kila uchao huku akionya kuwa usalama wao ni muhimu kwa ajili ya amani ya kudumu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa amepigwa picha kabla ya mazungumzo na wanakijiji na wapiganaji wa zamnai wanaoishi pamoja kama sehemu ya mchakato wa amani.
UNMVC
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa amepigwa picha kabla ya mazungumzo na wanakijiji na wapiganaji wa zamnai wanaoishi pamoja kama sehemu ya mchakato wa amani.

Umoja wa Mataifa uko nanyi

Katibu Mkuua amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushikaana na wananchi wa Colombia katika kusaidia mchakato wa amani na amewahakikishia wananchi kuwa atajadili na serikali juu ya suala la usalama na makazi.