Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali na upinzani wanaposhikamana hakuna linaloharibika

Picha: UM/Colombia
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, Jean Arnault(wa pili kutoka kushoto).

Serikali na upinzani wanaposhikamana hakuna linaloharibika

Amani na Usalama

Azma ya serikali ya Colombia na kikundi cha FARC ya kuhakikisha wanatekeleza makubaliano ya amani, imekuwa ni chachu ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Colombia, Jean Arnault amesema hayo leo akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokutana kupokea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo ya mwaka 2016.

Bwana Arnault ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa hivi karibuni kwa kiongozi mmoja wa FARC kwa tuhuma za kusafirisha madawa ya kulevya akisema kitendo hicho kiliibua zahma nchi humo. Hata hivyo..

(Sauti ya Jean Arnault)

“Wito kutoka kwa uongozi wa FARC hususan Rais wa chama Timoleon Jimenez,  wa kutaka watu watulie na kuendelea kutekeleza mkataba wa amani umekuwa ni muhimu sana katika kushughulikia shaka na shuku miongoni mwa wapiganaji wa zamani wa kikosi hicho kwenye maeneo ambako hivi sasa wanajumuishwa kwenye jamii.”

Image
Amani ndio jambo linalopigiwa chepuo. (Picha:MAKTABA-Mauricio Cardona/PNUD Colombia)

Hata hivyo ametaja mafanikio kuwa ni pamoja na hatua ya hivi karibuni ya mahakama ya kikatiba nchini Colombia ya kupitisha sheria juu ya hadhi ya upinzani, ambayo inatokana na moja ya vipengele kwenye makubaliano ya amani.

(Sauti ya Jean Arnault)

“Kipengele kinapatia upinzani fursa ya kutumia vyombo vya habari, kupata fedha na uwakilishi kwenye baraza la seneni na lile la wawakilishi kuelekea uchaguzi wa rais na makamu wa rais.”

Amegusia pia mchakato wa chaguzi za wawakilishi zilizofanyika tarehe 11 mwezi uliopita akisema mamilioni ya raia walishiriki na ilikuwa hatua muhimu kutoka kipindi cha mzozo kuelekea kwenye amani.

Halikadhalika Bwana Arnault amesema ilkuwa pia fursa kwa chama cha FARC kuondoka kwenye zama za silaha na kuingia kwenye siasa.

Uchaguzi wa rais nchini Colombia utafanyika wiki tano zijazo.