Mchakato wa amani nchini Colombia waanza kuzaa matunda: Arnault
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ujumbe wa Umoja huo nchini Colombia, Jean Arnault amewasilisha ripoti kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu mchakato wa amani kati ya serikali ya Colombia na waliokuwa waasi wa kundi la FARC nchini humo.
Katika ripoti yake, Bwana Renauld amesema “licha ya changamoto lukuki , mchakato wa amani nchini Colombia unaendelea kuzaa matunda mazuri na wakati uwakilishi wa FARC katika bunge ni hatua kubwa , ujumuishwaji katika maisha ya kawaida kwa wafuasi wa zamani wa FARC-EP ni shughuli ambayo haijakamilika , akisisitiza kwamba mafanikio ya mchakato huo bila shaka yatahitaji ari na rasilimali.”
Kwa mujibu wa ripoti yake “ lengo kuu la fursa za kuzalishia kipato kwa wapiganaji wa zamani 14,000 bado liko mbali sana kutekelezeka.” Hata hivyo amesema serikali imefanya uamuzi wa kukaribishwa wa kuendeleza msaada wa chakula katika maeneo ya mafunzo na mchakato wa kujumishwa katika jamii hadi mwisho wa mwaka 2018.
Ripoti pia imeainisha masuala mengine ambayo rais mpya mteule Iván Duque atakayeshika hatamu kuanzia Agost 7 mwaka huu atapaswa kuyashughulikia ili kumaliza mgawanyiko miongoni mwa watu wa Colombia. Masuala hayo ni pamoja na makundi mapya haramu, kuendelea kukua kwa biashara ya coca, na ghasia zinazoendelea katika baadhi ya maeneo hususan dhidi ya viongozi wa kijamii na watetezi wa haki za binadamu.