Mkakati wa wilaya moja bidhaa moja wainua viwanda vidogo Tanzania

22 Novemba 2021

Tanzania imeitikia wito wa kuimarisha viwanda vidogo vidogo kama njia mojawapo ya kufanikisha malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu, SDG ikiwemo kutokomeza umaskini.
 

Hatua hiyo ya Tanzania inajidhihirisha wazi wakati huu ambapo mwishoni mwa wiki dunia imeadhimisha siku ya viwanda barani Afrika ambapo  Umoja wa Mataifa unasema uko mstari wa mbele kusaidia kusongesha viwanda barani Afrika ili kufanikisha SDGs.

Katika taifa hilo la Afrika Mashariki, mwaka 1973 kulianzishwa shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo SIDO likiwa na majukumu makuu 6 ikiwemo kuongeza thamani ya rasilimali zilizoko nchini humo.

Katika kutekeleza jukumu hilo, SIDO ina mkakati uitwao Wilaya Moja Bidhaa moja ambapo akizungumza na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC Dar es salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji SIDO Shoma Kibende amesema “lengo la mkakati huu ni kuhakikisha rasilimali zinazozalishwa katika sehemu husika zinaleta tija kwa kuwa na viwanda lakini kutengeneza ajira na kuinua kipato cha wananchi wanaoishi hapo. Kwa hiyo kupitia mkakati huo sasa SIDO ilishirikana na Wizara na mamlaka za serikali za mitaa kuhamasisha kila wilaya kuwa na bidhaa inayotambulisha wilaya husika, na  hiyo bidhaa iwe ni ambayo rasilimali zake zinapatikana katika sehemu husika. Lengo likiwa bidhaa inayozalishwa pale iweze kuchakatwa na kuleta tija ya maendeleo ya sehemu husika.”

Bi. Shoma Kibende, Mkurugenzi wa SIDO akihusika na Uwekezaji na Masoko
Video Capture
Bi. Shoma Kibende, Mkurugenzi wa SIDO akihusika na Uwekezaji na Masoko

Mkakati wa wilaya moja bidhaa moja imefikia wilaya 115 za Tanzania Bara

Ametaja tayari wamefikia wilaya 115 za Tanzania Bara na wilaya zimechagua bidhaa zinazohusika ukienda Singida kuna zao la alizeni na asali. Arusha kuna maziwa na Mbeya kuna Mchele na Dodoma kuna Zabibu.

Bi. Kibende amesema SIDO pia inapatia mafunzo, teknolojia ili kuwezesha bidhaa hizo zichakatwe na pia kuwaungusha wenye viwanda na taasisi zinazotoa hati za ubora. “Tunawaunganisha na shirika la viwango Tanzania, TBS kupata ili wapate hati za kutambulika kuwa bidhaa ni bora na kisha waingie kwenye soko. Na pale kwenye uhitaji, SIDO inawapatia mtaji na pia kuwaunganisha na benki ili waweze kuchakata bidhaa hizo na kukidhi mahitaji ya soko.”

Mkurugenzi huyo wa Masoko na Uwekezaji SIDO pia amezungumzia changamoto ya vifungashio wa bidhaa akisema wanachofanya sasa wanawaunganisha na watengenezaji wa vifungashio walioko nchini na pia SIDO ina kituo chake kilichoko Dar es salaam ambacho hununua vifungashio na kuvisambaza. Amesema wanawaunganisha pia na watengenezaji wa vifungashio walio nje ya nchi huku wakihamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa vifungashio bora na kwa bei nafuu na vitakavyokidhi mahitaji ya wenye viwanda vidogo vidogo.

Mashine ya kukamua na kusagisha muhogo

Kuhusu mashine ya kukausha na kusagisha muhogo mbichi, Bi. Kibende amesema, “kweli SIDO tuna mashine ya kuchakata muhogo mbichi Mashine hii inapokea mihogo iliyomenywa na kuoshwa. Kazi yake ni kukata vipande vidogo vidogo na kisha inakamua, na kisha hukaushwa kwa siku mbili na kisha kusagishwa. Mashine hii inapatikana SIDO mkoani KIGOMA na ina uwezo wa kukamua kilo 750 kwa saa. Bei yake inaanzia shilingi milioni 2 na laki 5.”

Kuhusu kusambaza mashine nje ya nchi, Mkurugenzi huyo amesema mahitaji nchini ni makubwa na mashine nyingi zinatumika ndani ya nchi, lakini fursa zikitoka nje ya nchi wanashirikiana akisema,”tumeshashirikiana na Burundi katika teknolojia ya mawese. Tuko tayari kusambaza nje ya nchi iwapo mashine zitahitajika.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter