Nchi nyingi zataja ukosefu wa takwimu sahihi kuwa kikwazo cha kufanikisha SDGs

10 Julai 2018

Mwezi Julai ni mwezi wa mapitio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs , malengo ambayo ni ahadi iliyoridhiwa na mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.

Mkutano wa ngazi ya juu wa kutathmini utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ukiendelea jijini New York, Marekani, Tanzania imesema kama ilivyo kwa nchi nyingine, takwimu sahihi ndio kikwazo kikubwa cha utekelezaji wa ahadi hiyo ambayo ilipitishwa mwaka 2015.

Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Balozi Celestine Mushi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ameiambia idhaa hii kando ya kikao hicho kuwa jambo kubwa linaloibuka kwenye mjadala ni ukosefu wa takwimu sahihi kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya kaya.

Na zaidi ya kufikia ngazi hizo, takwimu zinazotakiwa ni zile ambazo zimenyumbuliwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo jinsia, elimu, maeneo na kadhalika.

UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yako 17 na yanayopitiwa mwaka huu kwenye mkutano ulioanza leo ni malengo 6.

Balozi Mushi amesema kwa Tanzani takwimu nyingi zinaishia wilayani tatizo likiwa ni  ukosefu wa rasilimali fedha, teknolojia, rasilimali watu na utaalamu hivyo amesema iwapo rasilimali watu na fedha zikipatikana, angalau wanaweza kuwa na takwimu zinazoanzia ngazi ya kaya hadi taifa.

Amefananisha takwimu sahihi na gari lenye dashibodi akisema ndio kipimo cha iwapo gari liko sawa au la.

"Tunapoandesha gari tunaangalia iwapo maji ni ya kutosha, kiwango cha joto ni sawa halikadhalika mwendokasi na mafuta, iwapo dashibodi haiko sawa basi ujue na gari lako halitakuwa sawa, vivyo hivyo takwimu sahihi na taifa," amesema Balozi Mushi.

Katika kikao hiki cha siku 8 nchi 47 zinawasilisha mapitio ya hiari ya utekelezaji wa SDGs ambapo Tanzania itafanya mawasilisho yake mwezi julai mwakani.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud