Tutaendelea kushirikiana na Afrika kusongesha maendeleo ya viwanda- UN

20 Novemba 2021

Katika kuadhimisha siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika, hii leo tarehe 20 mwezi Novemba mwaka 2021, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza azma ya umoja huo kushirikiana na viongozi na wakazi wa Afrika katika kuhakikisha maendeleo ya viwanda yanakuwa jumuishi na yanafungua njia ya ustawi na amani kwa wote.
 

Guterres amesema maendeleo ya viwanda jumuishi na endelevu ni muhimu wakati huu ambapo janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limeendelea kuwa na madhara kwa jamii na uchumi kila pahali.

Hata hivyo amesema wakati huo huo  uwekezaji katika kipindi cha kujikwamua baada ya COVID-19 ni fursa ya kizazi ya kuwa na marekebisho ya kijasiri nay a kasi ili kufanikisha ajenda 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu, kutokomeza umaskini, kupunguza ukosefu wa usawa na kujenga mnepo kwa tabianchi.

“Matumaini ya ustawi barani Afrika yamejikita katika kupanua wigo wa fursa kwa wanawake, wasichana na kuwekeza kwa vijana, kusongesha marekebisho kwenye sekta ya kilimo na viwanda, kujenga ubi ana ubunifu na kutekeleza kwa kina mkataba wa eneo la biashara huru barani Afrika,” amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu na zitasaidia kuondokana na utegemezi katika uchumi wa dunia hivi sasa uliogubikwa na utandawazi.

Siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1989 kupitia azimio namba 44/237 kwa lengo la kusongesha maendeleo ya viwanda barani  Afrika.

Na mwezi ujao wa Desemba kuanzia tarehe 2 hadi 4 huko Cabo Verde kutafanyika mkutano wa uchumi barani Afrika ukiwa na maudhui Kufadhili maendeleo ya Afrika baada ya COVID-19, mkutano ukilenga kuleta pamoja wadau mbali mbali wakiwemo watunga sera na sekta binafsi na watafiti kusaka mbinu za kupanua wigo wa vyanzo vya kufadhili maendeleo Afrika.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter