Baa la njaa labisha hodi Madagascar huku hatari kwa watoto ikiongezeka:WFP
Baa la njaa labisha hodi Madagascar huku hatari kwa watoto ikiongezeka:WFP
"Madagascar hivi sasa iko katika hatihati ya baa la njaa kwa mujibu wa tathmini ya vipimo vya hali cha chakula imefikia daraja la tano (IPC 5) katika baadhi ya maeneo au hali kama njaa, na hii kimsingi ndiyo hali pekee labda na ya kwanza ya njaa iliyochochewa na mabadiliko ya tabianchi duniani," amesema Arduino Mangoni, naibu mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP nchini Madagascar, akitumia tathmini za ukosefu wa chakula za IPC, ambazo ndio hutumika kupima kiwango cha usaidizi wa dharura unaohitajika.
Baada ya ziara ya hivi majuzi ya kuhuzunisha katika kituo cha lishe cha dharura Kusini mwa nchi hiyo, afisa huyo wa WFP amesema kuwa amekumbana na "hali ya kutia simanzi, ukimya ukitawala miongoni mwa watoto, hawana furaha tena wanakukodolea wewe macho na kwa sasa wengi ngozi zao zimesinyaa na wamesalia mifupa.”
Ameongeza kuwa "Nimekuwa nikifanya kazi na WFP katika nchi kadhaa katika bara hili, katika dharura kadhaa, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na huko Darfur, lakini sijawahi kuona watoto katika hali mbaya kama waliyo nayo hawa."
Ukame mbaya zaidi katika historia
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva kupitia zoom, Bw. Mangoni ameleeza kuwa taifa hilo la Madagascar limeathiriwa na ukame mkali zaidi katika kipindi cha miaka 40. "Wazee ambao tunawasaidia kusini nchi hiyo, wanaendelea kutuambia kuwa hili ndilo janga baya zaidi wanaliita 'Kéré', kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1981.”
Kwa jumla, amesema katika eneo la Malagasi watu milioni 1.3 wameorodheshwa kuwa katika daraja la IPC la 3, 4 na 5, kulingana na takwimu za mwisho zilizopo tangu mwezi Aprili.
Makadirio ya IPC yaliyofanyiwa marekebisho yatatolewa mwishoni mwa mwaka.
"Watu walio katika daraja la 3 na zaidi, ni karibu watu milioni 1.3 wakati huu tunapozungumza , na idadi hii ni ya juu kuliko watu waliokuwa katika daraja hilo mwaka 2016, wakati kulipozuka zahma ya El Niño," amesema afisa huyo wa WFP na kuongeza kuwa kwa kweli kumekuwa na tofauti ndogo kati ya daraja la tatu hadi la tano.
"Ikiwa tutaangalia makadirio ya miezi ijayo, hali inatisha sana", amesema, akibainisha kuwa mwelekeo wa kiwango cha tathimini ya chakula daraja la IPC 3, 4 na 5 tangu mwaka jana, kimepanda.
"Kwa hiyo, kama tukiangalia daraja la 4, karibu watu 200,000 walikuwa katika Daraja hilo muhula uliopita ambayo ni robo ya mwisho ya mwaka jana. Tuna karibu watu nusu milioni sasa, na makadirio ya watu katika kiwango cha darahja la 5 ni karibu 30,000, kati ya sasa na mwisho wa mwaka, wakati matokeo mapya ya IPC yatapatikana."
Njaa hii inaendeshwa na mabadiliko ya tabianchi
“Tofauti na njaa nyingine za kiwango cha darala la 5 la IPC duniani, huko Yemen, Sudan Kusini na Ethiopia/Tigray, ambazo zinatokana na migogoro, janga la Madagascar linatokana na mabadiliko ya tabianchi”, amebainisha afisa huyo wa WFP.
"Tuna matukio mabaya sana, kama vile ukame unaojirudia kila mwaka katika miaka mitano iliyopita, changamoto mpya ya jipya kimbunga cha mchanga pengine kilichosababishwa na mmomonyoko wa udongo, ukataji miti kwa miaka 20 hadi 30 iliyopita na kisha matokeo ya athari za COVID-29."
Kwa sababu ya athari za janga hili kwa utalii na ugavi, wanavijiji ambao walikuwa wametafuta kazi mijini wakati wa hali mbaya ya coronavirus">COVID-19 hawakuwa na chaguo hili tena, amesema Bw. Mangoni
Chakula, maji vimepanda bei
Watu pia wameshatumia mbinu zao zote za kawaida za kukabiliana na hali hiyo, kama vile kuuza vyombo vyao vya jikoni: "Kuna bei ya juu ya vitu, mfumuko wa bei unashangaza, hasa katika bei ya vyakula na maji. Halafu pia tuna ukosefu wa usalama, kuna jambo jipya limezuka linaitwa 'dahalo' ni majambazi wanaoharibu eneo hilo."
Kwa mujibu wa WFP, karibu Watoto 500,000 wa umri wa chini ya miaka mitano, wanaaminika kuwa na utapiamlo, 110,000 kati yao wanatarajiwa kuwa na unyafuzi kati ya sasa na Aprili 2022.
"Hawa ni watoto ambao wako katika hatari ya kufa kama hawatapatiwa msaada," Ameonya Bw. Mangoni akiongeza kuwa kupima athari za njaa kwa watoto wachanga ni jambo gumu, kwani mara nyingi vifo vyao havirekodiwi hasa kwa wale walio chini ya umri wa miezi sita.
Ili kuwasaidia wale wanaohitaji msaada zaidi, WFP tayari imeongeza mgao na programu za lishe; pia inapanga kufikia zaidi ya watu milioni moja walio katika la 3 hadi 5 la IPC kuanzia mwezi Desemba ambao ni kilele cha msimu wa muambo "hadi wakati wa mavuno mazuri yajayo", ambao unatarajiwa kuja Aprili 2022.
Ili kutoa msaada huu wa dharura kwa muda wa miezi sita ijayo, shirika hilo limetoa ombi la dola milioni 69.