Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa haraka wahitajika ili kuokoa mamilioni ya watu kutokana na njaa Yemen: UNICEF

Watoto waliokimbia makazi yao wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Mokha, Yemen.
© WFP/Annabel Symington
Watoto waliokimbia makazi yao wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Mokha, Yemen.

Msaada wa haraka wahitajika ili kuokoa mamilioni ya watu kutokana na njaa Yemen: UNICEF

Amani na Usalama

Bila hatua za dharura, mamilioni ya watu nchini Yemen wanaweza kukabiliwa na hatari zaidi ya njaa na utapiamlo, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto (UNICEF).

Shirika hilo limeongeza kuwa miaka minane ya vita vya kikatili vimewaacha takriban watoto milioni 11 wakihitaji msaada wa kibinadamu na wengi wa familia zao wakikabiliwa na utapiamlo mkali.

"Maisha ya mamilioni ya watoto walio katika mazingira magumu nchini Yemen yanasalia hatarini kutokana na matokeo yasiyoweza kufikirika, yasiyovumilika, ya vita kali na isiyoisha," amesema Peter Hawkins, mwakilishi wa shirika hilo nchini Yemen.

Bwana Hawkins ameongeza kuwa "UNICEF imekuwa hapa, ikitoa msaada unaohitajika sana katika kipindi cha miaka minane iliyopita, na hata kabla, lakini tunaweza tu kutoa msaada kiasi fulani kwa watoto na familia zilizoathirika bila amani ya kudumu."

Kijana mdogo akicheza wakati mama yake akipanga foleni katika eneo la maji kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao mjini Aden, kusini mwa Yemen.
© UNICEF/Moohialdin Fuad

Mzunguko wa kudumu wa kutokuwa na matumaini

Kwa mujibu wa shirika hilo la watoto mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen unatokana na mwaka 2015, wakati wanamgambo wa Houthi walipopambana na vikosi vya serikali inayotambulika kimataifa, na kuigawanya nchi hiyo, kuwafukuza mamilioni ya watu na kuharibu huduma muhimu na miundombinu.

Licha ya maafikiano ya muda mrefu na maendeleo ya hivi karibuni katika njia ya kuelekea amani, mkusanyiko wa mambo mkanganyiko umetokea, miaka minane ya mzozo mbaya zaidi,kuporomoka kwa uchumi, na mfumo mbovu wa usaidizi wa kijamii unaonyima huduma muhimu zinazoweza kuwaathiri wasiojiweza.

“Kati ya Machi 2015 na Novemba 2022, zaidi ya watoto milioni 2.3 wamekimbia makazi yao, 11,000 wameuawa au kujeruhiwa vibaya, zaidi ya 4,000 wameandikishwa wamesajiliwa na pande zinazopigana, na kumekuwa na mashambulizi zaidi ya 900 na matumizi haramu ya kijeshi kwa vituo vya elimu na afya. Hizi ni takwimu zilizothibitishwa, lakini takwimu halisi zinauwezekano wa kuwa kubwa Zaidi” limesema shirika la UNICEF.

Bwana Hawkins amesema "Baada ya miaka minane, watoto na familia nyingi huhisi kukwama katika mzunguko wa kudumu wa kukosa matumaini. Ukitembelea familia ambazo zimehamishwa kutoka kwenye makazi yao kwa zaidi ya miaka saba, unagundua kuwa kwa familia nyingi, hali yao kidogo imebadilika zaidi ya nyuso za watoto.”

Watoto wamekua wakijua kidogo sana kuhusu mambo mengine kwani kubwa wanalojiua ni migogoro, kuwapa watoto hawa fursa ya matumaini ya siku zijazo zenye amani ni jambo la maana sana. Ameongeza Hawkins.

Msichana mdogo akila banda lenye njugu wakati akitibiwa utapiamlo katika hostpial huko Sa'ana, Yemen.
© UNICEF/Mohammed Huwais

Tumaini, sio hofu

UNICEF inahitaji kwa dharura dola milioni 484 ili kuendeleza operesheni zake za kibinadamu za kuokoa maisha kwa watoto nchini Yemen mwaka 2023.

Ikiwa ufadhili hautapokelewa, UNICEF inaweza kulazimika kupunguza msaada wake muhimu.

Bwana Hawkins amesema. "Watoto wa Yemen wanapaswa kuwa na uwezo wa kutazama siku zijazo kwa matumaini, sio hofu. Tunatoa wito kwa pande zote kutusaidia kutoa matumaini hayo kwa kujitolea kwa watu wa Yemeni, na kuvuta nchi, na idadi ya watu waliochoka, kurudi kutoka ukingoni mwa kukata tamaa."