Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niliponea chupuchupu jangwani- Mhamiaji

Wahamiaji warejea nyumbani kwa hiari. Picha: IOM

Niliponea chupuchupu jangwani- Mhamiaji

Angalia hapa, hili ni jeraha la risasi ambayo nilifyatuliwa wakati nakimbia jangwani nikisaka maisha bora, ni kauli ya mmoja wa wasaka hifadhi ambaye amerejea nyumbani nchini Guinea baada ya kukumbwa na madhila huko Libya.

Msaka hifadhi huyo aliyejulikana kwa jina moja tu la Moussa amesema hayo baada ya kuwasili kwenye mji mkuu Conakry, chini ya mpango wa kurejea nyumbani kwa hiari unaofadhiliwa na shiirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM.

Moussa amerejea nyumbani wiki hii akisema aliponea chupuchupu kuuawa wakati wa lengo lake la kukimbilia Ulaya kucheza soka.

Ofisi ya IOM nchini Libya inasema tangu mwezi Oktoba wahamiaji zaidi ya elfu 11 wameshaondolewa nchini humo kwa hiari na kurejeshwa Nigeria, Guinea, Gambia na Mali.

Wahamiaji hao wameamua kurejea nyumbani kwa hiari badala kuishi kwenye mazingira magumu katika vituo vya kusubiria kufahamu hatma yao au kutumbukizwa kwenye ukatili.

Kwa mwaka huu ndege ya kwanza iliondoka jumatatu ikiwa na wahamiaji 142 kuelekea Gambia ambapo ndege nyingine inayokodishwa na IOM itaondoka jumatatu ijayo kuelekea Nigeria.

Mfumo wa utambuzi wa wahamiaji wa IOM, DTM, umebaini wahamiaji zaidi ya laki 4 nchini Libya, ambapo wengi wao wako kwenye miji ya Tripoli, Misrata na Almargeb huku ikikadiriwa kuwa idadi ya wahamiaji nchini humo ni kati ya Laki 7 na milioni 1.