Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa Tanzania nchini DRC watunukiwa nishani za Umoja wa Mataifa

Gwaride la walinda amani wa Tanzania nchini DRC kabla ya kutunukiwa  nishani za Umoja wa Mataifa
Kapteni Tumaini Bigambo
Gwaride la walinda amani wa Tanzania nchini DRC kabla ya kutunukiwa nishani za Umoja wa Mataifa

Walinda amani wa Tanzania nchini DRC watunukiwa nishani za Umoja wa Mataifa

Amani na Usalama

Walinda amani kutoka Tanzania, Kikosi cha 8 cha kujibu mashambulizi kinachohudumu katika ulinzi wa amani chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FIB MONUSCO wametunukiwa nishani ya Umoja wa Mataifa katika sherehe zilizopambwa kwa gwaride maalum lililoandaliwa na kikosi hicho. Afisa habari wa TANZBATT8, Kapteni Tumaini Bigambo alikuwepo katika hafla hiyo ana ametuandalia ripoti ifuatayo.

Walinda amani kutoka Tanzania, Kikosi cha 8 cha kujibu mashambulizi kinachohudumu katika ulinzi wa amani chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FIB MONUSCO wametunukiwa nishani ya Umoja wa Mataifa katika sherehe zilizopambwa kwa gwaride maalum lililoandaliwa na kikosi hicho cha TANZBATT 8. 

Sherehe hizo zimehudhuriwa na Kamanda wa vikosi vya ulinzi wa amani nchini DRC, Luteni Jenerali Afonso Da Costa na Mkuu wa Mafunzo ya utendaji kivita wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Jacob Mkunda. 

Luteni Kanali Fortunatus Nassoro ni Kamanda Kikosi wa TANZBATT 8 anasema, “kwa siku ya leo tuko hap ani siku ya kipekee kwa Umoja wa Mataifa kutunuku nishani kwa wanaulinzi wa amani wote ambao wako chini ya MONUSCO kama mnavyoiona hii hapa. Nishani au medali hizi hutolewa kwa maafisa na askari wote wa MONUSCO pale wanapomaliza kipindi cha miezi sita. Tangu tumefika hapa nchini DRC tumeweza kufanya shughuli mbalimbali na operesheni mbalimbali ambazo zimekuwa na mafaniko mafanikio makubwa sana angalau kupunguza makali ya vikundi vya waasi ambavyo vinasumbua sana raia. Kingine tunajaribu kuwa karibu na raia waliotuzunguka kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu pale tunapoweza, shuleni, kwa watoto yatima na kadhalika.” 

Naye Sajenti Jacob Mgonela, mlinda amani katikakikosi hicho cha TANZBATT 8 anasema, “katika baadhi ya majukumu yetu ya ulinzi wa amani tunafanya doria mbalimbali ambapo tumeanikiwa baadhi ya majukumu hayo tumefanya katika mji wa Mtwanga ambako wananchi wengi walikuwa wamehama katika mji huo lakini hatimaye kwa sasa wameweza kurejea. Kwa siku ya leo tuna furaha kwa sababu hii nishani ni kitu kwa sisi wanajeshi ni thamani moja kubwa sana kwa sababu tunapewa nishani baada ya kutekeleza majukumu ya amani kwa muda wa miezi sita.”  

Kwa upande wake Private Justina Manengwa anasema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kufika katika siku hii ya kutunukiwa nishani ambazo ni ishara ya ulinzi wa amani. Justina anasema, “tumekutana na changamoto nyingi lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia tumeweza kupata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa raia kwa juhudi za kuweza kuirejesha amani nchini DRC. Changamoto ni nyingi lakini tunaendelea kupambana nazo.”  

Hafla hiyo, pamoja na gwaride la kijeshi, ilipambwa pia na maonesho mbalimbali yakiwemo sarakasi na ngoma za kitamaduni, vyote hivyo vikifanywa na askari hao kutoka Tanzania.