Mtanzania atengeneza mashine ya Oksijeni ambayo haina ulazima kuwa na mtungi wa gesi

2 Agosti 2021

George Nyahende, raia wa Tanzania amebuni na kutengeneza mashine ya oksijeni ambayo ina sifa za kipekee ambazo anasema zinatokana na mazingira hususani ya vijiji vya Tanzania.

Kupitia katika mahojiano yaliyofanywa na Moses Mghase wa Kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC Dar es Salaam Tanzania, Bwana Nyahende ambaye ameipatia mashine yake hiyo jina lake Nyahende, ameeleza kinagaubaga namna alivyolifikia wazo hilo kwamba ni kutokana na kushuhudia kifo kilichotokana na nyoka.

Bwana Nyahende anasema, “kilichonisukuma ni kwamba wakati fulani nilitembelea sehemu fulani inaitwa Longido, Arusha. Kule kuna mama mmoja aligongwa na nyoka aina ya koboko au Black Mamba, sumu yake huwa inaathiri mfumo wa kupumua. Sasa baada ya muda alifariki na nilipoulizia wataalamu pale wakasema amefariki kwa sababu hawakuwa na mashine za kusaidia kupumua. Na nilipoangalia huko kijijini kulikuwa hakuna umeme wala nini, nikajua kama huyo ni mmoja ina maana kuna tatizo kubwa katika nchi nzima ndipo nilipoingiwa na wazo kwamba nijaribu kutengeneza hizo mashine lakini ambazo zitakuwa na uwezo wa kutumika hata kwenye sehemu hizo ambazo hazina nishati ya umeme.”

Mhandisi huyu anaeleza kuwa mashine anazozitengeneza zina uwezo wa kufanya kazi hata bila kutegemea mitungi ya gesi iliyobeba oksijeni kwani, “ni mashine rahisi ambazo zinaweza zikatumika katika mazingira yoyote na nimelenga zaidi vijijini kwa hiyo zinaweza zikatumia umeme wa nishati ya kawaida, umeme wa jua, au betri ya gari moja kwa moja au betri za redio zile nane za kawaida zinaweza zikaendesha hii mashine. Na inaweza ikatumia mifumo miwili ya hewa, ile ya Oksijeni iliyoko kwenye mitungi au hii hewa tunayovuta sisi, inaweza kubadilishwa ikachujwa na ikatumia kwa mgonjwa.”

Bwana Nyahede ambaye ni mkazi wa Arusha kaskazini mwa Tanzania, anasema kwa kadri atakavyodhidi kupata ufdahili au uwekezaji zaidi, ataendelea kuuboresha uvumbuzi wake huo, ili uende kusaidia watu kuanzia hospital hadi majumbani kwani ni mashine ambazo zinaweza kutumiwa katika mazingira yoyote hata kwa ngazi ya familia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter