Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania yashauriwa kujiunga na mpango wa chanjo wa COVAX 

Shughuli za ununuzi kwenye duka jijini Dar es Salaam, Tanzania wakati ugonjwa wa Corona ulivyoripotiwa Tanzania mwezi Machi mwaka huu.
UN News/ Stella Vuzo
Shughuli za ununuzi kwenye duka jijini Dar es Salaam, Tanzania wakati ugonjwa wa Corona ulivyoripotiwa Tanzania mwezi Machi mwaka huu.

Tanzania yashauriwa kujiunga na mpango wa chanjo wa COVAX 

Afya

Kamati iliyoundwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufanya tathmini juu ya Ugonjwa wa COVID-19 imependekeza taifa hilo kukubali Chanjo na kujiunga na COVAX ambao ni mkakati wa kimataifa wa kuhakikisha kila nchi inapata chanjo unaosimamiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.  

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Rais wa Tanzania Samia Hassan tume hiyo  imependekeza Tanzania kuzingatia taratibu za kisayansi katika kukabili janga la Covid 19 na kuruhusu vyombo vyake kuendeleza hatua za utoaji na matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kulingana na mwongozo wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO. 

Akiwasilisha ripoti hiyo Mwenyekiti wa Tume hiyo Profesa Said Aboud amesema tume hiyo pamoja na kupendekeza serikali kujiunga na Mpango wa COVAX, pia iyape kipaumbele makundi maalumu wakiwamo wahudumu wa Afya, wazee, wagonjwa, wahudumu wa vyombo vya  usalama na wasafiri wa nje. 

Aidha tume hiyo imeshauri Serikali itoe taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa wa COVID-19 sanjari na takwimu sahihi kwa umma na  pia kwa Shirika la Afya Duniani WHO ili ichukue hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za afua za kinga  katika ngazi zote ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo nchini Tanzania. 

Tume hiyo pia imeshauri Wizara yenye dhamana ya fedha na uchumi nchini Tanzania, ifanye tathmini ya kina ya athari za janga la COVID-19 na kuweka mpango madhubuti wa haraka wa sasa, wa muda wa kati na wa muda mrefu unaotekelezeka ili kukuza uchumi wa nchi.