Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Omicron ilichochea wimbi la Covid-19 barani Afrika lakini inapungua haraka 

Wanawake wakiwa wamejipanga mstari ili kupata chanjo dhidi ya Covid-19 nchini Malawi.
© UNICEF/ Thoko Chikondi
Wanawake wakiwa wamejipanga mstari ili kupata chanjo dhidi ya Covid-19 nchini Malawi.

Omicron ilichochea wimbi la Covid-19 barani Afrika lakini inapungua haraka 

Afya

Baada ya wimbi la ugonjwa wa Covid-19 lililodumu kwa takribani wiki sita, wimbi hilo la nne barani Afrika ambalo kimsingi lilichochewa na mnyumbuliko wa virusi vya corona kwa jina Omicron, sasa linapungua na hivyo kulifanya kuwa wimbi lililodumu kwa muda mfupi zaidi katika bara hilo ambako jumla ya maambukizi hivi sasa tangu kuibuka kwa ugonjwa huo limezidi milioni 10. Imeeleza taarifa ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika iliyotolewa hii leo Brazzaville nchini Congo.  

WHO inasema maambukizi ya kila wiki yaliongezeka katika siku saba hadi tarehe 9 Januari kutoka wiki iliyokuwa imetangulia. Kusini mwa Afrika, ambako kulishuhudiwa ongezeko kubwa la maambukizi wakati wa wimbi, taarifa njema ni kuwa kumerekodiwa kupungua kwa maambukizi kwa asilimia 14 katika wiki iliyopita. Afŕika Kusini, ambapo mnyumbuliko wa Omicron uliripotiwa kwa mara ya kwanza, imeshuhudia  kushuka kwa asilimia 9 kwa maambukizi ya kila wiki. Kanda za Afrika Mashariki na Kati pia nazo zimeshuhudia kupungua kwa maambukizi. Hata hivyo, Afrika Kaskazini na Magharibi inashuhudia kuongezeka kwa maambukizi, huku Afrika Kaskazini ikiripoti ongezeko la asilimia 121 katika wiki iliyopita ikilinganishwa na ile wiki iliyopita. 

“Katika bara zima, hata hivyo, vifo viliongezeka kwa asilimia 64 katika siku saba zilizomalizika tarehe 9 ya mwezi huu wa Januari ikilinganishwa na wiki iliyotangulia hasa kwa sababu ya maambukizi miongoni mwa walio katika hatari kubwa. Pamoja na hayo, vifo katika wimbi la nne ni chini kuliko mawimbi ya awali. Idadi ya wagonjwa wanaolazwa imesalia chini kwa mfano  nchini Afrika Kusini katika vitanda 5600 vya chumba cha wagonjwa mahututi, ni asilimia 9 tu ya vitanda hivyo imelaliwa na wagonjwa wa Covid-19.” Inaeleza WHO lakini ikionya kuwa, “wakati bara la Afrika linaonekana kukabiliana na wimbi la hivi karibuni la janga hili la Corona, waliochanjwa bado ni wachache. Ni takriban asilimia 10 tu ya wakazi wa Afrika wamechanjwa kikamilifu." Usambazaji wa chanjo kwa bara umeboreshwa hivi karibuni, na WHO inaongeza msaada wake kwa nchi ili kufikisha dozi kwa watu wengi zaidi barani humo.