Tanzania inavyokabili janga la corona

26 Mei 2020

Ni miezi miwili na zaidi sasa tangu Tanzania itangaze mgonjwa wake wa kwanza wa virusi vya COVID-19.  Tangu tarehe 16 mwezi wa tatu mwaka huu mengi yamejiri nchini Tanzania kufuatia kuzuka kwa janga la ugonjwa huo unaoathiri dunia nzima.

Kulingana na takwimu za CDC na za serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, idadi ya wagonjwa walioathirika na ugonjwa huo nchini Tanzania imefikia 509 na vifo vilivyoripotiwa na serikali ya Tanzania ni 21 hadi hivi sasa.  Wagonjwa waliopona ni 183.

Hatua za Tanzania kudhibiti COVID-19

Jitihada zilizofanywa na uongozi wa nchi hii ni pamoja na kutoa Elimu kwa umma kuhusu mlipuko wa ugonjwa huu mpya wa Corona, dalili zake zilielezewa pamoja na namna ya kuepuka maambukizi.  Jamii kwa mfano imeelimishwa kuhusu umuhimu wa kunawa mikono, kutumia vitakasa mkono, kuepuka misongamano kwa kuzingatia umbali baina ya mtu mmoja na mwingine. Ndani ya mwezi uliopita, kumekuwa na mwenendo wa kutumia barakoa kwa ajili ya kuzuia maambukizi zaidi pale ambapo mtu anakohoa au kupiga chafya.

Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa kinadhihirisha kwamba kwa kiasi kikubwa kumekuwa na ufahamu mkubwa kuhusu baa la Corona ama COVID-19.

Shule na vyuo vilifungwa hapo awali ili kuzuia mlipuko kuenea Zaidi, hivi sasa vinatarajiwa kufunguliwa tarehe moja June.

Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam nchini Tanzania
World Bank / Sarah Farhat
Wanafunzi wa wakiwa darasani katika shule ya msingi ya Zanaki jijini Dar es Salaam nchini Tanzania

Ambacho hakikufanyika

Hata hivyo Tanzania, haikufuata mkondo wa nchi nyingi wa kufunga uchumi na shughuli zote za kijamii.  Ni baadhi tu ya shughuli zilifungiwa kama michezo na mikusanyiko ya arusi ama maeneo ya starehe. 

Shughuli zingine ziliendelea kama kawaida huku rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwahimiza wananchi kuchapa kazi na kuondoa hofu huku wakichukua tahadhari.

Dkt. Magufuli aliiongoza nchi kufanya maombi dhidi ya Corona. Wananchi wengi waliitikia wito.  Makanisa na madhehebu mbalimbali yaliamua kwa hiari kuchukua hatua za kupunguza utaratibu Fulani Fulani waliouzoea ili kuzuia kueneza maambukizo Zaidi lakini kamwe hawakufunga shughuli za ibada.

Magari ya kusafirisha abiria al maarufu kama daladala zilipewa utaratibu wa kuingiza abiria na wa watu kukaa bila kubanana.  Japo kulikuwa na milolongo mirefu kuingia ndani ya magari hayo, ilileta heshima ya kutokuenea kwa kasi zaidi kama ilivyotabiriwa na Shirika la Afya Duniani-WHO, kwamba watu wengi zaidi wangepoteza maisha.

Kwa watu wengi wanaimani kwamba kweli Mungu amesimama na Watanzania. Huenda utamaduni wa Watanzania wa kunawa mikono umesaidia kupunguza athari za ugonjwa huo hatari.  Vile vile, Tanzania na nchi zingine za barani Afrika zilijifunza kutoka kwa yaliyojiri Ulaya na kwingineko ambapo Ugonjwa ule ulitikisa Zaidi.

Utafiti wa kutafuta Chanjo ya virusi vya Corona unaendelea
Unsplash
Utafiti wa kutafuta Chanjo ya virusi vya Corona unaendelea

Hivi karibuni, watanzania wengi zaidi wamekuwa wakijifukiza kwa kutumia majani ya miti asilia kama mikaratusi, miarobaini, mipera na kadhalika kwa kuongozwa na wataalamu wa afya ya mitishamba

Wanaotambulika kitaifa.  Nchi ya Tanzania pia imeunga mkono dawa ya kupunguza makali inayosadikiwa kutibu ugonjwa wa COVID-19 iliyotolewa na rais wa Madagascar Ange Rajoelina.

Wakati jitihada nyingi duniani zinaendelea kutafiti na kupata chanjo kwa ajili ya Corona ama COVID-19, nchini Tanzania wananchi wanaendelea kuchukua tahadhari huku wakiendelea na shughuli zao.

Hatua za nchi jirani

Nchi nyingi za jirani ikiwemo, Rwanda, Zambia, Uganda na Kenya zilifunga mipaka yake na Tanzania kwa kuhofia maambukizi Zaidi.  Waandishi wa Habari kutoka nchini Kenya, mwanzo waliilaumu Tanzania kwanini haikufunga uchumi wake-yaani ‘Lock down’  baada ya nchi hizo kufungia shughuli za kila siku palitokea sintofahamu na baadhi ya watu walipoteza maisha wakijaribu kujitetea.

Tanzania ni nchi ambayo hata huko nyuma ilijitolea sana kusaidia nchi zingine za barani Afrika zipate uhuru wao kutoka kwa wakoloni.  Kwa mara nyingine tena, rais wa nchi hiyo alielezea kwamba hakuweza kufunga mipaka kutokana na Tanzania kutegemewa na nchi zisizokuwa na mipaka.  Alielezea nchi hizo hutegemea Tanzania kwa vitu kama chakula, nyama.

Hivi karibuni nchi zilezile zilizoibeza Tanzania zimelazimika kuanza kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao.  Rais wa Tanzania alisema iwapo Tanzania ingefunga uchumi wake ingekuwa wapi?  Alielezea ya kwamba watu wengi hutegemea kipato cha kila siku ndipo wapate chakula.

 

Wanawake wanaofanya kazi ya kufikisha mafunzo kwa wanawake wasema wanahofia wanawake wenzao ambao wanakaa manyumbani bila kwenda popote wakati huu wa janga la corona.
© UNFPA Syria
Wanawake wanaofanya kazi ya kufikisha mafunzo kwa wanawake wasema wanahofia wanawake wenzao ambao wanakaa manyumbani bila kwenda popote wakati huu wa janga la corona.

Japokuwa maambukizi bado yapo, inaelezewa kwamba idadi ya wagonjwa wanaopokelewa kwenye taasisi za afya nchini Tanzania zimepungua kwa kiasi kikubwa.  Kumekuwa na ripoti za madereva wanaosafiri masafa marefu kupimwa katika maeneo ya mipaka ya nchi za Uganda na Kenya na baadae kubainika kwamba wana virusi vya COVID-19.  Hali hii imeleta mtafaruku kuhusu jinsi ambavyo wagonjwa wanapimwa nchini Kenya na kwa mfano wengi wao wamelalamikia vipimo kutokuwa sahihi.  Swala hili la vipimo liliwahi pia kuzungumziwa na rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alisema alibaini kuna mapungufu kwenye zana za kupimia Corona kwani vyombo vya ulinzi na usalama viliwahi kupima kwenye maabara papai, Mafuta ya gari na kware na kubaini kwamba zina virusi vya Corona hali iliyodhihirisha vifaa vya kupimia kutoka China huenda vilikuwa batili.

Changamoto mipakani

Ndani ya wiki hii iliyopita, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu, alizungumzia suala la mgogoro wa mipakani uliosababishwa na madereva na piaamesisitiza umuhimu wa kurejesha mahusiano mema na kwamba magari za kusafirisha mizigo hayakupigwa marufuku kuingia nchini Kenya. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amezungumza pia na Rais wa Tanzania kuhusu sakata hili la madereva na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama na watawala wa mikoa inayopakana kukutana na kusuluhisha changamoto zilizojitokeza.

Tanzania imekuwa na msimamo wa kitofauti na hii imeelezewa na Dkt. Magufuli kuwa inatokana na nchi yake kuwa huru na yenye kujiongoza yenyewe bila kushurutishwa yaani kwa lugha ya kigeni husema ni, sovereign state’.

 

Jumapili ya tarehe 17 Mei, 2020, Rais Magufuli aliagiza shughuli za michezo kuanza tena pamoja na shughuli za utalii ambapo aliruhusu ndege zianze kutua na kusafirisha watalii.  Siku chache baadae  tarehe 21 Mei rais huyo aliagiza vyuo zifunguliwe pamoja na wanafunzi wa kidato cha sita wa shule za sekondari kurejea kwa ajili ya maandalizi ya mitihani.

Kila nchi ina mapokeo yake ya janga hili.  Kwa Tanzania, watu wanaendelea na kazi huku wakichukua tahadhari. Tanzania pia inategemea kuwa na uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu.

Taarifa hii imeandaliwa na Stella Vuzo @UNIC Dar es salaam

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter