Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu milioni 275 walitumia mihadarati 2020:UNODC Ripoti

Ripoti ya Matumizi ya dawa duniani 2021
Source: UNODC
Ripoti ya Matumizi ya dawa duniani 2021

Takriban watu milioni 275 walitumia mihadarati 2020:UNODC Ripoti

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC imeonya kwamba idadi ya watu wanaotumia mihadarati duniani inaongezeka na kwamba mwaka jana 2020 pekee duniani kote takriban watu milioni 275 walitumia mihadarati, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 22 tangu mwaka 2010. 

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa ofisi hiyo ambao pia unatoa mtazamo wa jumla wa soko la mihadarati duniani pamoja na athari zake kwa afya za wat una maisha yao katika mtazamo wa janga la corona au COVID-19
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya dawa za kulevya ya dunia ya UNODC 2021, matumizi ya bangi ya yameongezeka mara nne katika baadhi ya sehemu za dunia zaidi ya miongo miwili iliyopita, wakati asilimia ya vijana ambao walijukulia madawa ya kulevya kama ni hatari ilishuka kwa asilimia 40. 
 
Pengo hili la mtazamo bado lipo licha ya ushahidi kwamba matumizi ya bangi yanahusishwa na aina mbalimbali za athari za afya na madhara mengine, hasa kati ya watumiaji wa muda mrefu.  
Aidha, nchi nyingi zimeelezea kuongezeka kwa matumizi ya bangi wakati wa janga la COVID-19. 
 
"Mtazamo wa chini wa hatari ya matumizi ya madawa ya kulevya umehusishwa na viwango vya juu vya matumizi ya dawa hizo, na matokeo ya ripoti ya dawa za kulevya ya dunia ya UNODC ya 2021 yinaonyesha haja ya kuziba pengo kati ya mtazamo na hali halisi kwa kuelimisha vijana na kulinda afya ya umma," amesema mkurugenzi mtendaji wa UNODC Ghada Waly. 

Muuguzi akimpatia dawa ya Methadone Mraibu wa Heroin nchini Vietnam
UNODC/PTRS/Nick Danziger
Muuguzi akimpatia dawa ya Methadone Mraibu wa Heroin nchini Vietnam


 
  Athari ya kiuchumi ya janga hilo. 

Ripoti hiyo inasema janga la COVID-19 limetumbukiza watu zaidi ya milioni 100 katika umaskini uliokithiri, na limesababisha ukosefu wa ajira na kuchochea zaidi pemngo la usawa, wakati dunia ikipoteza ajifra milioni 114 mwaka 2020.  
Hali ya matatizo ya afya ya akili pia inaongezeka duniani kote. Sababu hizi zina uwezo wa kuinua ongezeko la matatizo ya matumizi ya mihadarati. 
 
Aidha, mabadiliko yameshaanza kubainika katyika mifumo ya matumizi ya dawa za kulevya wakati wa janga la corona, ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya bangi na matumizi yasiyo ya matibabu ya dawa za usingizi.  
Changamoto za kiuchumi pia zinauwezekano wa kuharakisha upanuzi wa soko kwa dawa hizo. 
 


  Jukumu la teknolojia 
  

Sambamba na hilo, Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamejikwamua haraka kutoka kwenye athari za mwanzo zilizosababishwa na vizuizi vya kukabiliana na COVID-19 na sasa wanafanya kazi tena katika viwango vya kabla ya janga hilo, wakiongozwa na kuongezeka kwa utumiaji wa teknolojia na malipo ya pesa za sarafu. 
 
Upatikanaji wa mihadarati na uuzaji mtandaoni pia umekuwa rahisi zaidi kuliko wakati wowote, na masoko makubwa ya dawa kwenye wavuti za kinyemela sasa yana thamani ya dola milioni 315 kila mwaka.  
Shughuli za uuzaji wa mihadarati kwa njia isiyo ya ana kwa ana kama vile kupitia barua poepe, pia zinaongezeka, mwenendo ambao huenda umechapuzwa na janga hilo. 
 
Ubunifu wa haraka wa kiteknolojia, pamoja na wepesi na jinsi wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya ambao wanatumia njia mpya za mtandaoni kuuza dawa za kulevya na vitu vingine, kunaweza kuongeza upatikanaji wa dawa haramu. 
Mwenendo mzuri 
 
Kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia wakati wa janga la COVID-19 pia kumesababisha ubunifu katika huduma za kuzuia madawa ya kulevya na matibabu, kwa njia ya mifano rahisi zaidi ya utoaji wa huduma kama vile dawa kwa njia ya simu (telemedicine), kuwezesha wataalamu wa afya kufikia na kutibu wagonjwa wengi zaidi. 
 
Wakati huo huo, idadi ya huduma mpya ya kisaikolojia (NPS) inayojitokeza kwenye soko la kimataifa ilianguka kutoka 213 mwaka 2013 hadi 71 mwaka 2019.  
Matokeo haya yanaonyesha mifumo ya udhibiti wa kitaifa na kimataifa imefanikiwa katika kupunguza kuenea kwa NPs katika nchi za kipato cha juu, ambapo mwenendo huo uliibuka kwanza miaka kumi iliyopita. 
 
Ripoti pia imegundua kwamba matumizi ya aina mbili za kitabibu za afyunyi dawa zinazotumiwa kutibu watu wenye matatizo ya matumizi ya mihadarati aina ya opioid, methadone na buprenorphine, yamezidi kupatikana, kama matibabu ya msingi ya sayansi kwa kiasi kikubwa. 

Matumizi ya dawa kwa watu wenye umri mkubwa yamekuwa yakiongezeka haraka ikilinganishwa na makundi ya vijana kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa
Unsplash/Sharon McCutcheon
Matumizi ya dawa kwa watu wenye umri mkubwa yamekuwa yakiongezeka haraka ikilinganishwa na makundi ya vijana kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa


  Kuganga yajayo 
  

"Mihadarati inagharimu maisha," anahitimisha mkuu wa UNODC. "Katika wakati ambao kasi ya habari mara nyingi inaweza kuzidi kasi ya inaweza kuzidi kasi ya kuthibitisha, janga la COVID-19 limetufundisha kwamba ni muhimu kuachana na kelele na kuzingatia ukweli, somo ambalo tunapaswa kuzingatia ili kulinda jamii kutokana na athari za madawa ya kulevya. " 
 
Uzinduzi wa Ripoti ya Madawa ya Dunia ya 2021 umekuja katika kuelekea siku ya kimataifa dhidi ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu, itakayoadhimishwa hapo tarehe 26 Juni. 
 
Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2021 ya kampeni inayoongozwa na UNODC ni "Sambaza ukweli juu ya mihadarati, okoa maisha" ili kufikia ulimwengu bila ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya.