Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inabadili mfumo wa usafirishaji haramu wa mihadarati :UNODC Ripoti

Mihadarati iliyopatina Nchini South Africa :UNODC
UNODC
Mihadarati iliyopatina Nchini South Africa :UNODC

COVID-19 inabadili mfumo wa usafirishaji haramu wa mihadarati :UNODC Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu, UNODC imesema janga la virusi vya corona au COVID-19 limeathiri utaratibu wa usafirishaji haramu wa mihadarati hususan kwa njia ya anga na hivyo kuwafanya wasafirishaji haramu kusaka njia mbadala.

Ripoti hiyo ya UNODC imesema kwamba hatua zinazotekelezwa na nchi mbalimbali kupambana na janga la COVID-19 zimevuruga usafirishaji haramu wa mihadarati kwa kutumia ndege sambamba na kupunguza biashara hiyo kwa kiasi kikubwa au kuongeza kuingiliwa na kuzuiliwa kwa biashara hiyo kupitia usafirishaji wa njia ya ardhi.

Pia imesema mitandao mingine ya usambazaji wa mihadarati hiyo imebanwa na kuingiliwa na wafanyabiashara sasa wanalazimika kutafuta njia mbadala ikiwa ni pamoja na kutumia usafiri wa baharini.

Ripoti hiyo ya utafiti wa “masoko, na mwenendo wa biashara ya mihadarati wakati huu wa janga la COVID-19” imesema "dawa za kulevya kama vile methamphetamine (TAMKA METHAFENTAMIN)huwa zinasafirishwa mabara yote duniani kwa njia ya anga kuliko aina zingine za mihadarati. Hivyo vikwazo vya usafiri wa anga vinaweza kuwa na athari kubwa sana kwa dawa hizo haramu. Shehena kubwa ya cocaine imekuwa ikisafirishwa kwa njia ya bahari na kutokana na hatua za kupambana na corona shehena hizo zimekuwa zikigundulika baharini hasa Ulaya"

 Heroin imekuwa ikisafrishwa kwa njia ya barabara, lakini kutokana na COVID-19 njia ya bahari inaonekana kutumika zaidi hususan kupitia bahari ya Hindi.

Nayo bangi ripoti imesema huenda usiathirike kwa kiwango kikubwa kama cocaine na heroin hasa ukizingatia kwamba uzalishaji wake kwa kiasi kikubwa hufanyika karibu na masoko ya wateja.

Katika matumizi ripoti  inasema nchi nyingi zimeripoti uhaba wa dawa hizo za kulevya katika ngazi ya ununuzi wa rejareja, lakini kwa mihadarati kama heroin kwa mfano ripoti inasema uhaba wa kusambazwa unaweza kufanya kuwa na matumizi hatari, kama vile madawa ya kujitengezenea nyumbani na kuonya kwamba watumiaji wa heroin huenda wakabadili mwelekeo na kuingia kwenye dawa zingine kama fentanyl. 

Hatari nyingine itokanayo na uhaba wa mihadarati ofisi hiyo imesema ni ongezeko la kujidunga sindano na kushirikiana sindano hizo ambapo vyote vina hatari ya kusambaza magonjwa kama virusi vya ukimwi (VVU) na ukimwi, Homa ya ini aina ya C na virusi vya COVID-19.

Na ripoti imeonya kwamba kudorora kwa uchumi kunakosababishwa na COVID-19, kuna uwezekano wa kusababisha mabadiliko makubwa katika soko la mihadarati.