Watumiaji wa mihadarati waongezeka huku COVID-19 ikivuruga soko la dawa hizo:UN Ripoti

25 Juni 2020

Takriban watu milioni 269 walitumia mihadarati duniani kote mwaka 2018 ikiwa ni asilimia 30 zaidi ya ilivyokuwa mwaka 2009 huku watu wengine milioni 35 wakiathirika na kuugua magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya- imesema ripoti mpya kuhusu mihadarati duniani iliyotolewa leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu, UNODC.

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo pia imetathimini athari za janga la corona au COVID-19 kwenye soko la mihafdarati, ingawa athari zake bado hazijafahamika kikamilifu, vikwazo vya mpakani na vikwazo vingine vinavyohusina na janga la corona tayari vimesababisha upunguza wa madawa mitaani, na kuchangia ongezeko la bei na kupunguza ubora wa dawa hizo.

Masikini ndio waathirika wakubwa

Ripoti hiyo ambayo imetathimini hali ya mihadarati duniani kote pia imesema ongezeko la ukosefu wa ajira na kupungua kwa fursa kulikosababishwa na janga la corona kunaathiri kwa kiasi kikubwa watu masikini na kuwaweka hatarini Zaidi kutumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa mihadarati hiyo na kilimo cha dawa hizo ili kujipatia fedha.

Akizungumzia ripoti hiyo mkurugenzi mtendaji wa UNODC Ghada Waly amesema “Makundi ya watu walio hatarini na waliotengwa, vijana, wanawake na masikini ndio wanaolipa gharama kubwa matatizo ya mihadarati duniani.janga la COVID-19 na kudorora kwa uchumi kumeendelea kutoa tisho la hatari ya mihadarati wakati mifumo yetu ya kiafya na kijamii imeelemewa kupita kiasi na jamii zetu zinahaha kukabiliana na hali hii. Tunahitaji serikali zote kuonyesha mshikamano mkubwa na kutoa msaada kwa nchi zinazoendelea na Zaidi ya yote kukabiliana na usafirishaji haramu wa mihadarati na pia kutoa huduma zenye Ushahidi kwa matatizo ya kiafaya yanayosababishwa na mihadarati na magonjwa mengine ili kuweka kufikia malengo ya maenedeleo endelevu, kuchagiza haki na kutomwacha yeyote nyuma.”

Wasafirishaji haramu wasaka mbinu mpya

Kutokana na janga la COVID-19 mkurugenzi huyo mtendaji amesema wasafirishaji haramu wa mihadarati sasa itabidi watafute njia nyingine na mipango mipya, na pia shughuli za usafirishaji kupitia njia za panya na posta zinaweza kuongezeka licha ya usafirishaji kupitia posta kuingiliwa kiasi na COVID-19.

Ripoti inasema janga hili la COVID-19 limesababisha pia kuwepo kwa uhaba wa afyunyi hali ambayo inaweza kuchangia watu kuanza kusaka mbadala wa dawa za kulevya kama vile pombe, madawa mengine ambayo ni hatari na kuchanganya madawa ambayo sio hali.

Mbali ya hayo huenda matumizi ya hatari zaidi yakaibuka kwa sababu watumiaji kubadili mwenendo na kuingia kwenye sindano au kujidunga kupita kiasi.

Ikiangalia athari zaidi za janga la corona ripoti inasema kwamba endapo serikali zitachukua hatua kama ilivyochukua wakati wa mdororo wa uchumi kwaka 2008 ambapo walipunguza bajeti ya masuala yanayohusiana na madawa basi uingiliaji wa hatua kama za kuzuia matumizi ya mihadarati na tabia zinazoendana, huduma za tuba za waathirika wa madawa hayo, utoaji wa dawa za kudhibit mauamivu kwa waathirika na kubadili hatua ya matumizi ya kupita kiasi ya afyunyi vinaweza kuathirika vibaya.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter