Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi ya Mariam: Dawa za kulevya zilinifanya kupoteza mtoto na mume

Hepatitis C huathiri kwa kiasi kikubwa makundi yaliyotengwa ikiwa ni pamoja na watu wanaojidunga dawa za kulevya.
Unsplash/Diana Polekhina
Hepatitis C huathiri kwa kiasi kikubwa makundi yaliyotengwa ikiwa ni pamoja na watu wanaojidunga dawa za kulevya.

Simulizi ya Mariam: Dawa za kulevya zilinifanya kupoteza mtoto na mume

Afya

Tatizo la dawa za kulevya duniani ni suala tata ambalo linaathiri mamilioni ya watu duniani kote. Watu wengi wanaotumia dawa za kulevya hukumbana na unyanyapaa na ubaguzi, jambo ambalo linaweza kudhuru zaidi afya yao ya kimwili na kiakili na kuwazuia kupata usaidizi wanaohitaji.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu UNODC inatambua umuhimu wa kuchukua mtazamo unaozingatia watu kuhusu sera za dawa za kulevya, kwa kuzingatia haki za binadamu, huruma na mazoea yanayotegemea ushahidi. 

Miongoni mwa shuhuda nzuri katika jamii ni kuwa wale waliotumia dawa za kulevya wanaweza kurejea kwenye afya zao na maisha yao ya awali iwapo wataacha na kukaaa kwenye vituo vya matibabu ya uraibu na matibabu. Mmoja ya mifano mizuri ya waliorejea katika hali yao ya awali ni binti Mariam. 

Soundcloud

Mariam ni nani?

Mariam, sio jina lake halisi, raia wa Pakistan binti aliyetoka kwenye familia bora, ana umri wa miaka 25 kwa sasa na anasimulia ilikuwaje mpaka akadumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya. 

Nilivyokuwa na miaka 18 niliolewa katika familia yangu, baada ya kuolewa mume wangu alikuwa anakaa nami mara chache sana, mara nyingi nilikuwa mwenyewe. Katika kipindi hiki nilikuwa mjamzito na wakwe zangu walikuwa wananifanyia vitu vingi sana vibaya, nilipata hasira na ndipo nilipoanza matumizi ya dawa za kulevya.”

Hatimaye Mariam alipata talaka, na hali ikazidi kuwa mbaya. 

“Kule kukaa peke yangu kulinifanya kuwa mraibu wa dawa za kulevya, siwezi hata kufikiria uharibifu ambao nimefanya kutokana na dawa za kulevya, kila mara nikikaa na kufirikiri, mwili wangu una kakamaa.”

Na sasa akaenda kuanza maisha upya yeye na mtoto wake 

“Nilipoteza familia, nilipoteza afya yangu, nivigumu kufikiria hali niliyokuwa nayo kabla ya kuja katika kituo cha uraibu. Nakumbuka nilikodi chumba na nikawa nasema uongo, nalalamika kuwa chumba kina aina fulani ya ulevi, lakini kuna mtu akawaambia familia yangu kuwa binti yenu anatumia aina fulani ya ulevi, hali ilikuwa mbaya kaka yangu alivyokuja na namna alivyonikuta, nilikuwa nimeisha kabisa, sikuwa na hela sikuwa na chochote, nilikuwa namuacha mtoto wangu mwenyewe amejilalia hapo mchana na usiku maana nilikuwa sijiwezi kwa ulevi.“

Jambo jema kwa Mariam, familia yake haikumtenga bali ilimueleza kuwa huu ni ugonjwa na unaweza kupatiwa matibabu na kumpeleka katika kituo cha uraibu na matibabua ya mihadarati.

“Hapa nimepata matibabu kwa miezi mitatu, na nimekubali kubadili vitu vingi kwasababu siwezi kueleza vitu ambavyo nimeharibu sababu ya dawa za kulevya, nimeharibu maisha yangu, familia yangu, ninasikia huzuni kila nikifikiria nimepoteza heshima ya kaka yangu, sipo na mtoto wangu , mume wangu ameniacha lakini sasa nashukuru na nafurahi maana napata matibabu na naendelea vizuri, uraibu ni ugonjwa na unatibika.”

Na mara baada ya kuachana na dawa za kulevya mume wa Mariam amemsamehe na kukubali kumrejea na anapata msaada kutoka kwa familia yake. 

“Sikuwa shupavu nilivyokuja hapa, lakini sasa niña nguvu na nimejifunza mengi na ninamuomba Mungu nisirudi tena kwenye umasikini ule.”