Takribani watu 6,000 wamekimbia makazi ya dharura kutokana na mashambulizi DRC- UNHCR 

4 Juni 2021

Mashambulizi makali yanayotekelezwa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces ADF, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC yamewalazimisha watu 5,800 kukimbia mara kadhaa katika makazi ya watu waliotawanywa katika jimbo la Ituri Mashariki mwa nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na msemaji wa UNHCR Babar Baloch kwa waandishi wa Habari, tarehe 31 Mei mwaka huu mashambulizi yaliyofanyika wakati mmoja katika makazi tofauti ya watu waliotawanywa na vijiji kadhaa karibu na miji ya Boga na Tchabi yalikatili maisha ya raia 57 wakiwemo Watoto 7 ambao walipigwa risasi na wengine kukatwa kwa mapanga. 

Katika mashambulizi hayo UNHCR imesema watu wengine wengi walijeruhiwa, 25 kutekwa nyara huku wenginemakazi zaidi ya 70 na maduka yalichomwa moto. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa katika mji wa Boga pekee wanawake, wanaume na Watoto 31 waliuawa. 

Baadhi ya manusura wamewaambia washirika wa UNHCR kwamba ndugu zao wengi waliteketezwa kwa moto wakiwa hai katika nyumba zao. 

Shirika hilo la wakimbizi limekasirishwa na kusikitishwa sana na ukatili huu wa hivi karibuni unaofanywa na makundi yenye silaha Mashariki mwa DRC  na Baloch ameongeza kuwa “Tunatoa wito wa kuongeza kasi ya usalama katika jimbo hilo kulinda maisha ya raia ambayo wengi wao wameshambuliwa na kulazimishwa kukimbia mara kadhaa, na tunarejea ombi letu kwa pande zote kuheshimu masuala ya kibinadamu ikiwemo makazi ya watu waliotawanywa.” 

Kwa kuhofia mashambulizi zaidi maelfu wameukimbia mji wa Boga na viunga vyake bila chochote isipokuwa nguo tu walizovaa. 

Ingawa baadhi ya watu waliokimbia bado wanalala msituni au katyika maeneo ya wazi wengi wamekaribishwa na kuhifadhiwa na familia ambazo ni masikini ambazo tayari zinahaha kwa kutokuwa na rasilimali za kutosha na wengine wamesaka hifadhi katika makanisa ambayo kwa sasa yamefurika. 

UNHCR imeongeza kuwa hali ya kutokuwepo kwa usalama katika eneo hilo inaathiri kazi za wahudumu wa kibinadamu. 

Vituo vya afya vimelazimika kufungwa kwa mud ana kusitisha shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kuhamisha wafanyakazi wake kutoka Ituri na kuwapeleka Bunia. 

Ofisi za mmoja wa washirika wa UNHCR ziliporwa na kuwakosesha msaada muhimu maelfu ya wakimbizi. 

Hivi sasa timu za UNHCR ziko katika eneo hilo kutathimini mahitaji ya watu waliolazimika kukimbia na jamii zinazowahifadhi. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter