Mashambulizi mashariki mwa DRC yafurusha watu 20,000 

16 Julai 2021

Mashambulizi dhidi ya raia huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yamesababisha watu 20,000 kukimbia makazi yao licha ya hatua ya Rais Felix Tshisekedi ya kutangaza hali ya hatari katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini tarehe 6 mwezi Mei mwaka huu. 

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Babar Baloch, amewaambia waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi ya kwamba tangu tarehe 22 mwezi uliopita wa Juni, waasi wa kikundi cha Alliance Democratic Force, ADF wamedaiwa kuua kikatili raia 14 na kujeruhi wengine wengi katika mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini. 

Bwana Baloch amesema katika shambulio hilo la kwanza katika kipindi cha miaka miwili waasi hao pia walipora mali na kuchoma moto nyumba. 

“Tunatoa wito wa hatua za haraka zichukuliwe ili kulinda raia wakati huu ambapo vikundi vilivyojihami vinaendelea kushambulia na kutishia raia licha ya Rais Tshisekedi kutangaza hali ya hatari,” amesema Bwana Baloch. 

Amesema kutokana na vitisho vya waasi hao, wananchi wana hofu kbwa na hawana imani na vikosi vya usalama kwa kuzingatia hakikisho la usalama walilopatiwa baada ya hatua mpya za ulinzi kutangazwa. 

Mashambulizi ya hivi karibuni yamelazimu watu kukimbilia maeneo ya usalama mashariki mwa Beni na vile vile yanasababisha kuvurugika kwa shughuli za kiuchumi, kijamii na kielimu. 

Bwana Baloch amesema hofu yao ni kwamba licha ya juhudi zao za usaidizi wa kibinadamu, DRC inaendelea kuwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu kwa kuzingatia dharura ya tarehe 22 mwezi Mei ya mlipuko wa mlima Nyiragongo uliofurusha watu makwao. 

Ghasia huko Kivu Kaskazini zimefurusha takribani watu milioni 2 katika kipindi cha miaka miwili pekee. 

Kwa sasa UNHCR na wadau inasadia waliofurushwa kusajiliwa na kutathmini mahitaji yao. 

Mwaka 2020 wakimbizi wa ndani zaidi ya 100,000 walipatiwa msaada ilihali mwaka huu pekee tayari watu 14,000 wamepatiwa msaada na mahitaij bado ni makubwa. 

Shirika hilo linasema fedha zaidi zinahitajika kwa kuzingatia kuwa ombi lake la operesheni nchini DRC la dola milioni 205 limefadhiliwa kwa asilimia 36 pekee. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter