Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ADF yakatili maisha ya mamia ya watu na kutawanya wengine 40,000 DRC:UNHCR 

Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/UN0377403/Roger LeMoyne
Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Droro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

ADF yakatili maisha ya mamia ya watu na kutawanya wengine 40,000 DRC:UNHCR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UHNCR limetoa onyo kuhusu kuongezeka kwa idadi ya mashambulizi yanayofanywa na makundi yaliyojihami dhidi ya raia kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.  

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, USwisi msemaji wa UNHCR, Babar Baloch amesema "tangu Januari mshambulizi yametajwa kutekelezwa na kundi la waasi la ADF ambalo limeua takriban watu 200 na kujeruhi  makumi ya watu na kusababisha watu  wengine wapatao elfu 40 katika eneo la Beni, Kivu Kaskazini pamoja na vijivi karibu na jimbo la Ituri kukimbia makwao.   

UNHCR imesema katika kipindi cha chini ya miezi mitatu, ADF imevamia vijiji 25, imeteketeza makumi ya nyumba na kuteka zaidi ya watu 70. Hii ni pamoja na vifo 465 vinavyotajwa kutekelezwa na waasi hao wa ADF mwaka 2020.  

Kwa ujumla, mashambulio na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu pia unaendelea katika maeneo mengine ya jimbo la Kivu Kaskazini.  

Kulingana na UNHCR, "sababu kuu za mashambulio haya zimeripotiwa kuwa ni kulipiza kisasi kunakofanywa na makundi yaliyojihami kwa silaha dhidi ya operesheni za kijeshi, kusaka chakula na dawa, na shutuma dhidi ya jamii kushiriki kutoa habari kuhusu maeneo walipo ADF." 

Dola milioni 2 zinahitajika hara kwa ajili ya Beni 

Kufuatia mashambulio ya hivi karibuni, watu wamelazimika kuhamishwa kwa nguvu makwao  na kishakusaka hifadhi katika miji ya Oicha, Beni na Butembo, katika eneo la Beni. Wengi wao walikimbia kwa pikipiki. 

Wengi wa wakimbizi hawa wa ndani ni wanawake na watoto. "Wanaume wanapendelea kukaa mahali pa kulinda mali zao, na hivyo kujiweka katika hatari ya kushambuliwa zaidi," amefafanua msemaji wa UNHCR. 

Ikumbukwe kwamba kabla ya wimbi hili la hivi karibuni la "maelfu ya watu kutawanywa ", UNHCR inakadiria kuwa wakimbizi wa ndani 100,000 tayari walihitaji ulinzi na msaada kupata makazi huko Beni. 

Kwa kina zaidi, watu hawa waliohamishwa wanaishi katika "hali mbaya, bila makazi, chakula, maji au huduma za afya. Katika muktadha wa Ebola na Covid-19, ukosefu wa upatikanaji wa vyoo, maji ya kunywa, sabuni na bidhaa za usafi wa hedhi ni jambo la kutia wasiwasi sana," Bwana Baloch ameongeza, akibainisha kuwa na familia hazina vitu muhimu vya kutosha kama blanketi au magodoro . 

Walikokimbilia, UNHCR imeweza kujenga zaidi ya makaazi  kwa familia 43,000 Mashariki mwa DRC mwaka jana.  

Mwaka huu wa 2021, kutokana na fedha zilizopo  sasa, ni familia 4,400 tu ndizo zitaweza kusaidiwa kutoka kwa mamia ya maelfu wanaohitaji msaada. 

UNHCR kwa hivyo inahitaji haraka dola $ 2 milioni ili kuimarisha ulinzi na hatua za  kibinadamu huko Beni, Kivu Kaskazini na eneo la Irumu huko Ituri.  

Hivi sasa, kati yad ola milioni 33 zinazohitajika na UNHCR kukidhi mahitaji ya Mashariki mwa DRC zimefadhiliwa kwa 5.5% pekee.