Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa chakula waikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati – WPF/FAO

Mataifa MINUSCA unatekeleza mradi wa matokeo ya haraka ya kuwezesha jamii kupata kipato na kujinusuru na umaskini
UN/MINUSCA - Hervé Serefio
Mataifa MINUSCA unatekeleza mradi wa matokeo ya haraka ya kuwezesha jamii kupata kipato na kujinusuru na umaskini

Uhaba wa chakula waikumba Jamhuri ya Afrika ya Kati – WPF/FAO

Msaada wa Kibinadamu

Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa basi Jamhuri ya Afrika ya kati – CAR ndani ya miezi michache itaingia katika baa kubwa la njaa kwa kuwa asilimia 47 ya wananchi wake sawa na watu Milioni 2.2 wengi wao waliopo vijijini wana uhaba mkubwa wa chakula na wengine wakiuza mifugo yao na kuwaondoa watoto wao shule ili waweze kumudu kununua chakula

Taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Bangui nchini CAR hii leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la mpango wa chakula duniani WFP na la chakula na kilimo FAO nchini humo, imeeleza miongoni mwa hatua za haraka zinazohitaji kuchukuliwa ni pamoja na kuondoa vizuizi vya kufikisha misaada ya kibinadamu katika jamii zinazotegemea misaada hiyo ili kuishi

Mwakilishi mkazi wa FAO nchini CAR, Perpetua Katepa-Kalala amesema wananchi wa Afrika ya kati wameishi kwa mateso makubwa ya vita kwa miongo kadhaa na kumekuwa na ongezeko la uhaba wa chakula takriban kila mwaka sasa.

Lakini kwa sasa hali ya ukosefu wa chakula imekuwa mbaya zaidi. Janga la Corona limefanya mipaka kufungwa na masoko kufungwa au kuwekwa vizuizi, hii imeathiri upatikana wa chakula na kupandisha bei ya chakula. Hivi karibuni tutakuwa kwenye msimu wa Mwambo ambao unafanya barabara za mchanga kutotumika. Usambazaji wa chakula, mbegu za kilimo na mahitaji mengine muhimu utakuwa mgumu zaidi. Ni muhimu tuchukue hatua za haraka,” amesema Bi. Katepa-Kalala

Naye mwakilishi mkazi wa WFP nchini humo Aline Rumonge, amesema msimu wa mwambo unaendana na msimu wa mazao na matunda kuanza kuota, kipindi ambacho chakula kinakuwa haba kabla ya mavuno kuanza.

 Hivyo amesema, “tunahitaji kuvunja huu mzunguko wa vita na njaa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati. hatujawahi kuona watu wengi wakisukumwa hivi hadi katika kona ya mwisho ya kuokoa Maisha yao – zaidi ya watu nusu milioni wanakaribia kabisa kukumbwa na baa la njaa. tunatoa wito wa dharura kuomba hatua zichukuliwe sasa kuokoa Maisha kabla yakuchelewa sana.”

Kufungwa kwa barabara ya Bouar - Garoua Boulai karibu na mpaka wa CAR na Cameroon kulikofanywa  na vikosi vyenye silaha mwishoni mwa mwaka jana kumeathiri usambazaji za bidhaa muhimu na misaada ya kibinadamu kwa miezi kadhaa.