Ukata wazidisha ongezeko la njaa miongoni mwa wakimbizi:WFP

Ukata wazidisha ongezeko la njaa miongoni mwa wakimbizi:WFP
Mamilioni ya wakimbizi wanakabiliwa na mustakbali wa sintofahamu na janga la njaa wakati athari za janga la corona au COVID-19 likiendelea kuathiri bajeti za misaada na hivyo kuathiri operesheni za dharura za misaada kwa wakimbizi limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP.
Katika ujumbe wake kuelekea siku ya wakimbizi duniani inayoadhimishwa kila mwaka Juni 20 shirika hilo limesema ukata wa ufadhili Afrika Mashariki na Kusini na pia Mashariki ya Kati umelazimisha kupunguza mgao wa chakula kwa watu walio hatarini zaidi ambao maisha yao yanategemea msaada wa shirika hilo ili kuishi wakiwemo wakimbizi.
Kupunguza mgao
WFP inasema Afrika Mashariki pekee karibu robo tatu ya wakimbizi mgao wao wa chakula umepunguzwa kwa asilimia 50 na Kusini mwa Afrika wakimbizi nchini Tanzania ambao wanategemea msaada wa WFP pekee mgao wao umekatwa kwa theluthi moja, na ukata wa fedha za msaada kwa wakimbizi wa Syria inamaanisha kwamba wakimbizi 242,000 walioko nchini Jordan wanaweza kukatwa kabisa na msaada ifikapo mwisho wa mwezi Agosti endapo hakuna fedha zozote za msaada zitakazopokelewa.
"Tunachoweza kuona ni athari za COVID-19 kwa ufadhili wa serikali za wafadhili na hii inaathiri vibaya uwezo wetu wa kuchukua hatua na kusaidia watu wengine walio katika mazingira magumu zaidi duniani," amesema Margot van der Velden, mkurugenzi wa dharura wa WFP na kuongeza kuwa "Maisha ya watu waliotengwa zaidi ulimwenguni yapo kwenye hatarini na tunawahimiza wafadhili kutowapa migongo wakimbizi wakati wanawahitaji zaidi msaada wao."

Kuepuka kupunguzwa kwa msaada wa chakula zaidi ama kupitia mgao uliopunguzwa au kuwatenga watu kutoka kwenye msaada kabisa, ufadhili wa kutosha unahitajika angalau mwezi mmoja kabla ya mapumziko yanayotarajiwa ya mtiririko wa chakula kwa nchi zinazopokea wakimbizi.
Pengo la ufadhili linapanuka
Mapungufu ya ufadhili yanaongezeka sanjari na kuongezeka kwa bei ya chakula na fursa chache kwa wakimbizi za kusaidia kupata msaada wao wa chakula wakati uchumi usio rasmi unapungua kwa sababu ya masharti yya kujikinga na COVID-19 limeongeza shirika la WFP.
Wakati huo huo, idadi ya watu wanaohitaji sana msaada inaongezeka ulimwenguni wakati mizozo, majanga na kuporomo kwa uchumi kunasababisha ongezeko la kiwango cha njaa.
WFP na mashirika mengine ya kibinadamu wanakabiliwa na kufanya uchaguzi wa kinyama.
Nchini Rwanda, WFP imetoa msaada wa chakula kwa kuwalenga na kuwapa kipaumbele wale tu wanaohitaji zaidi msaada.
Pamoja na hayo, WFP inasema ufadhili ni mdogo sana hata wale walio katika mazingira magumu zaidi bado hawapati mgao kamili, ambao huja kwa njia ya msaada wa pesa.