Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF Burundi yatoa mafunzo ya Ujuzi kwa wasichana 

Biashara mtandaoni imeimarika wakati wa janga la COVID-19.
Unsplash/rupixen
Biashara mtandaoni imeimarika wakati wa janga la COVID-19.

UNICEF Burundi yatoa mafunzo ya Ujuzi kwa wasichana 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaendesha programu maalumu ya mafunzo kwa wasichana nchini Burundi kwa lengo la kupunguza pengo la wanawake kwenye sayansi na stadi za kazi ambapo wahitimu arobaini kutoka majimbo manne wamepatiwa vyeti vya kuhitimu.  

Naibu mwakilishi mkazi wa UNICEF Burundi, Nathalie Meyer akizungumza katika mahafali hayo amesema ujuzi waliopata katika programu hii utawanufaisha wanajamii wanaowazunguka na kuongeza idadi ya viongozi wanawake 

Siku nzuri ya kila mwanafunzi kutunukiwa cheti cha uhutimu wa mafunzo, mafunzo yanayoendana na karne ya 21 yenye lengo la kupunguza pengo la kidigitali, na pia kujikita katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati. 

Naibu muwakilishi wa UNICEF nchini Burundi Nathalie Meyer anasema miongoni mwa mafunzo waliyotoa ni uongozi pamoja naa stadi za kazi ili kuwawezesha wasichana wanaoshiriki katika programu kuweza kujiajiri na kuajiri wengine pamoja na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao.

Kwakweli huu ni mwanzo wa safari, ni mwanzo wa safari yetu, tumewapa mafunzo ya kuwajengea uwezo, ya ujasiriamali, lakini pia wanajua ku code kwenye mitandao mbalimbali na pia kuwaonesha kuwa wanaweza kufanya kazi za kiume au kitamaduni kazi zile zinazoonesha kuwa ni za wanaume. 

Meyer ameongeza kuwa wanafunzi hawa wamepokea mafunzo hayo kwa morali mkubwa

Wamekuwa wavumilivu sana, wenye shauku na kwakweli watakuwa mawakala muhimu wa mabadiliko, wakirudi kwenye jamii zao, wataweza kufundisha wengine vitu walivyo jifunza na kuchangia kule pia kuwafundisha wasichana wengine na wanajamii wengine.  

Kauli ya Meyer imeungwa mkono na wahitimu ambapo Ndayikeza Viola mwenye umri wa miaka 23 kutoka Jimbo la Mwaro anasema jamii ikae tayari kuona mabadiliko. 

“kwa mfano tumejifunza kujenga nyumba, sisi wasichana mara nyingi huwa tunajidharau wenyewe na tunajisemea kuwa hatuwezi kufanya kazi hizo na hizi kwasababu zipo kwa ajili ya wanaume , kwa ujuzi huu tuliopatiwa , nitawadhibitishia kuwa tunao uwezo wa kufanya na nitawafundisha mabinti wengine.

Mabadiliko yatagusa kila kona ya maisha ambao Nisengwe Cecili mwenye umri wa miaka 17 kutoka Rumoge, anasema mbinu mpya za utunzaji wa mazingira zitasaidia jamii yake. 

“Tunaweza kupanda miti pembezoni ya mto hii itazuia mmomonyoko wa udongo, lakini pia kutengeneza mkaa ambao ni rafiki kwa mazingira, shukurani kwa mbinu za kisasa tulizofundishwa za kuchanganya unga wa muhogo , udongo na chenga za mkaa” 

Wahitimu hawa wanatarajiwa kurudi katika jamii zao na kuangalia mazingira yaliyowazunguka na kuona ni namna gani wanaweza kutumia ujuzi walioupata kutatua changamoto zilizopo.