Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umasikini umepungua duniani lakini bado kuna zaidi ya watu Bilioni 1.1 ni masikini

Covid-19 imesukuma watu kutumbukia katika umasikini zaidi.
© UNICEF/Fazel
Covid-19 imesukuma watu kutumbukia katika umasikini zaidi.

Umasikini umepungua duniani lakini bado kuna zaidi ya watu Bilioni 1.1 ni masikini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP limetoa ripoti yake kuhusu hali ya umaskini duniani inayoonesha ingawa nchi 25 zimepunguza nusu ya umasikini ndani ya miaka 15 bado kuna watu bilioni 1.1 wanasalia katika umasikini. 

Taarifa ya UNDP iliyotolewa leo kutoka New York Marekani imeeleza kuwa takwimu kutoka nchi 110 zilizofanyiwa makadirio kupitia kipimo cha MPI kwa kushirikiana na mpango wa maendeleo wa Chuo Kikuu cha Oxford, OPHI yamedhihirisha kuwa kupunguza imasikini kunawezekana ingawa athari kamili za janga la COVID-19 bado hazijaonekana. 

Kulingana na toleo hili la mwaka 2023, watu bilioni 1.1 kati ya bilioni 6.1 (zaidi ya 18%) wanaishi katika umaskini mkubwa wa pande nyingi katika nchi 110. 

Watu 5 kati ya 6 ni masikini

Barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara idadi yao ni milioni 534 na Asia Kusini idadi ni milioni 389 hii ni takriban watu watano kati ya watu sita ni maskini.

Takriban theluthi mbili ya watu wote maskini (watu milioni 730) wanaishi katika nchi za kipato cha kati, na hivyo kufanya hatua katika nchi hizi kuwa muhimu katika kupunguza umaskini duniani.

Ingawa nchi zenye kipato cha chini zinajumuisha 10% tu ya watu waliojumuishwa katika MPI, lakini nchi hizi ndizo ambapo 35% ya watu wote maskini wanaishi.

Siphiwe Nxumalo mfanyakazi wa kujitolea wa shirika la WFP Ewsatin alirejea nyumbani ili kuwasaidia watoto yatima na walio hatarini wanaohaha kwa umasikini
© WFP/Theresa Piorr
Siphiwe Nxumalo mfanyakazi wa kujitolea wa shirika la WFP Ewsatin alirejea nyumbani ili kuwasaidia watoto yatima na walio hatarini wanaohaha kwa umasikini

Watoto

Watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanachangia nusu ya watu maskini (milioni 566). 

Kiwango cha umaskini miongoni mwa watoto ni 27.7%, wakati kati ya watu wazima ni 13.4%. 

Umaskini unaathiri zaidi maeneo ya vijijini, huku 84% ya watu wote maskini wakiishi vijijini. Maeneo ya vijijini ni maskini kuliko maeneo ya mijini katika mabara yote ya dunia.

MPI inatoa mwanga juu ya utata wa umaskini - ambapo viashiria tofauti vinachangia uzoefu wa watu wa umaskini kwa njia tofauti, ikitofautiana kutoka kanda moja hadi kanda nyingine ambayo ni ndogo, na kati na ndani ya jamii. 

 

COVID-19 imekwamisha tathmini kamilifu

Mkurugenzi wa Ofisi ya Ripoti ya Maendeleo ya Kibinadamu wa UNDP Pedro Conceição amesema licha ya mwelekeo huu wa kutia moyo, ukosefu wa takwimu baada ya janga la COVID-19 kwa zaidi ya nchi 110 kumezuia uelewa wao wa athari za janga hilo kwa umaskini.

"Tunapofikia katikati ya Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, tunaweza kuona wazi kwamba kulikuwa na maendeleo thabiti katika kupunguza umaskini wa pande nyingi kabla ya janga hili. Athari za janga hili katika nyanja kama vile elimu ni muhimu na zinaweza kuwa na matokeo ya kudumu.” 

Amesema ni muhimu kuimarishwa kwa juhudi za kufahamu vipimo vilivyoathiriwa zaidi, na hivyo kuhitaji kuimarishwa kwa ukusanyaji wa takwimu na juhudi za sera za kurejesha upunguzaji wa umaskini kwenye mstari.

Pamoja na ukosefu wa takwimu sababu ya janga la COVID-19 kuleta changamoto katika kutathmini matarajio ya haraka, uchambuzi wa mwelekeo kutoka mwaka 2000 hadi 2022, uliolenga nchi 81 zilizo na takwimu linganifu kwa wakati, unaonesha kuwa nchi ya India imekuwa na mafanikio makubwa kwa watu zaidi ya milioni 415 kuondoka kwenye umasikini ndani ya kipindi cha miaka 15 (2005/6–19/21).

Idadi kubwa ya watu waliondolewa kutoka kwenye umaskini nchini China, watu milioni 69 kati ya mwaka 2010-2014 na Indonesia watu milioni 8 kati ya mwaka 2012-2017.

Nazo nchi 25 zilifanikiwa kupunguza nusu ya vingo vyao ya kimataifa vya MPI ndani ya miaka 15, kuonesha kuwa maendeleo ya haraka yanaweza kufikiwa. Hizi ni pamoja n anchi ya Cambodia, China, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo -DRC, Honduras, India, Indonesia, Morocco, Serbia, na Vietnam.

Wazazi wa Rani wanaishi chini ya kiwango cha umasikini na wanategemea programu ya mlo wa mchana ya WFP.
WFP/Isheeta Sumra
Wazazi wa Rani wanaishi chini ya kiwango cha umasikini na wanategemea programu ya mlo wa mchana ya WFP.

Tathmini ya zile walizokusanya takwimu

Mkurugenzi wa OPHI katika Chuo Kikuu cha Oxford Sabina Alkire amesema wanashangaa kuona "Uhaba wa kustaajabisha wa takwimu kuhusu umaskini wa pande nyingi na ni mgumu kueleweka, achilia mbali kuhalalisha katika dunia inayumbayumba chini ya mafuriko ya takwimu na inayo jiandaa kwa enzi ijayo ya ukuaji wa kidijitali. “

Tunatoa wito kwa wafadhili na wanasayansi wa masuala ya takwimu kufanya mageuzi kwenye ukusanyaji wa takwimu ili watu masikini waweze kufuatiliwa na kusaidiwa.

Hata hivyo kwakuzingatia nchi chache ambapo takwimu ilikusanywa pekee mwaka wa 2021 au 2022 ambazo ni Mexico, Madagascar, Cambodia, Peru, na Nigeria, kasi ya kupunguza umaskini imeonekana kuwa inaweza kuendelea wakati wa janga la COVID-19.

Nchi za Cambodia, Peru, na Nigeria zilionesha punguzo kubwa katika vipindi vyao vya hivi karibuni, na hivyo kutoa matumaini kwamba maendeleo bado yanawezekana. Nchini Cambodia, matukio ya umaskini yalipungua kutoka 36.7% hadi 16.6%, na idadi ya watu maskini ilipungua, kutoka milioni 5.6 hadi milioni 2.8, yote ndani ya miaka 7.5, ikiwa ni pamoja na miaka ya janga (2014-2021/ 22).

Kwa msisitizo mpya wa ukusanyaji wa takwimu, UNDP wameeleza watapanua uwanda wa kuangalia umasikini ili kujumuisha athari za janga hili kwa watoto. 

Katika zaidi ya nusu ya nchi walizozifanyia tathmini, hakukuwa na punguzo kubwa la kitakwimu katika umaskini wa watoto au thamani ya MPI ilishuka polepole zaidi miongoni mwa watoto kuliko miongoni mwa watu wazima katika angalau kipindi kimoja. Hii inaonesha kuwa umaskini wa watoto utaendelea kuwa suala la dharura, hasa kuhusiana na mahudhurio ya shule na utapiamlo.